Latest Posts

MAREKANI YASITISHA MSAADA, KIKOSI CHA KENYA HAITI CHATARAJIWA KUKUMBWA NA CHANGAMOTO

Hatima ya kikosi cha usalama cha kimataifa kinachoongozwa na Kenya nchini Haiti imeingia katika sintofahamu baada ya Marekani kutangaza kusitisha mchango wake wa kifedha kwa mfuko wa Umoja wa Mataifa unaolifadhili. Hatua hii inazua wasiwasi juu ya mustakabali wa operesheni hiyo, ambayo tayari inakabiliwa na changamoto za kifedha na vifaa.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric, alisema Jumanne kuwa Marekani imetoa agizo la kusitisha mara moja mchango wake wa dola milioni 13.3 kwa mfuko wa Multinational Security Support (MSS), ambao ndio unafadhili kikosi kinachoongozwa na Kenya.

“Tumepokea taarifa rasmi kutoka kwa Marekani ikiomba kusitishwa mara moja kwa mchango wao,” alisema Dujarric, akisisitiza kuwa mfuko huo tayari ulikuwa unakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha.

Hatua hii ya Marekani inafuatia sera mpya za Rais Donald Trump za kupunguza misaada ya nje, ikiwa ni pamoja na mipango ya kusitisha shughuli za Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID).

Mwezi Oktoba 2023, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliridhia kuundwa kwa MSS ili kusaidia mamlaka za Haiti kukabiliana na magenge ya wahalifu yanayodhibiti maeneo makubwa ya nchi hiyo. Hata hivyo, upungufu wa fedha na vifaa umeathiri utekelezaji wake, huku Kenya ikiwa nchi inayobeba mzigo mkubwa wa operesheni hiyo.

Kenya ilikuwa imejitolea kuongoza kikosi hicho kwa kushirikiana na mataifa mengine, huku Rais William Ruto akiahidi kusaidia kurejesha utulivu Haiti. Kufikia sasa, Kenya imetuma maafisa 800 kati ya wanajeshi 2,500 waliotarajiwa, lakini hatua ya Marekani kuondoa ufadhili wake inaweza kuchelewesha au kudhoofisha operesheni hiyo zaidi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alionya mwishoni mwa Januari kuwa kuchelewesha msaada kwa Haiti kunaweza kusababisha magenge kuteka mji mkuu, Port-au-Prince.

“Tunahitaji fedha zaidi, vifaa na askari wa kimataifa kwa haraka. Kuchelewa zaidi kunaweza kusababisha kuporomoka kwa taasisi za usalama za Haiti na kuruhusu magenge kudhibiti eneo lote la mji mkuu,” alionya Guterres.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Haiti, Jean-Victor Harvel Jean-Baptiste, aliongeza kuwa nchi hiyo inakabiliwa na “changamoto kubwa” zinazotishia uhai wa taifa.

Mwaka 2024 pekee, zaidi ya watu 5,626 wameuawa nchini Haiti kutokana na ghasia za magenge, ongezeko la takriban watu 1,000 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia. Zaidi ya wananchi milioni moja wameyakimbia makazi yao, idadi ambayo ni mara tatu ya mwaka uliopita.

Hadi sasa, mfuko wa Umoja wa Mataifa wa kusaidia MSS umefanikiwa kukusanya dola milioni 110 pekee, kiasi ambacho hakitoshi kukidhi mahitaji ya operesheni hiyo.

Marekani ilikuwa imechangia dola milioni 15 kwenye mfuko huo ikiwa ni mchango wa pili kwa ukubwa baada ya dola milioni 63 za Canada huku dola milioni 1.7 zikiwa tayari zimeshatolewa.

Mbali na mfuko huo, chini ya uongozi wa Joe Biden, Marekani pia ilitoa msaada wa zaidi ya dola milioni 300 moja kwa moja kwa MSS, ikiwa ni pamoja na magari ya kivita kadhaa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!