Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, amewataka wananchi wenye sifa kujitokeza kugombea nafasi za uongozi wa Serikali za Mitaa kwa kuchukua na kurudisha fomu kuanzia tarehe 26 Oktoba hadi 1 Novemba, 2024.
Waziri Mchengerwa ametoa wito huo wakati wa tathmini ya uandikishaji wa wapiga kura katika uchaguzi huo, mara baada ya kujiandikisha katika kituo cha Michikichini, Kijiji cha Umwe Kaskazini, wilayani Rufiji.
Waziri amewasihi Watanzania wenye sifa kuchangamkia fursa hiyo na kusisitiza kuwa, kampeni za uchaguzi zifanyike kwa staha na kulinda utulivu wa taifa.
“Zoezi la kuchukua na kurudisha fomu litafanyika kuanzia Oktoba 26 hadi Novemba 01, 2024, na ni muhimu kampeni zijayo zijikite katika siasa za kistaarabu ambazo zitadumisha amani nchini,” amesema Mchengerwa.
Aidha, Waziri amewapongeza wananchi, wanachama wa vyama vya siasa, na wapenzi wao kwa kuonesha ukomavu wa kisiasa wakati wa zoezi la uandikishaji. Amesisitiza umuhimu wa kuendelea na siasa za hoja badala ya siasa za ugomvi, ambazo zinaweza kuhatarisha amani ya taifa.
Mchengerwa pia ametoa wito kwa vyombo vya usalama kuendelea kulinda amani na utulivu wakati wa mchakato mzima wa uchaguzi, akibainisha kuwa, ni jukumu la vyombo hivyo kuhakikisha usalama wa wananchi ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huu muhimu wa Serikali za Mitaa.
Sambamba na hayo, Waziri amewasihi wasimamizi wa uchaguzi na wadau wote kuzingatia sheria na kanuni za uchaguzi, ili mchakato mzima uwe wa haki na uwazi, na uendeshwe kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
Uchaguzi huo umepangwa kufanyika tarehe 27 Novemba, 2024, ambapo wananchi watapata fursa ya kutimiza haki yao ya kikatiba.