Wananchi wameendelea kunufaika kupitia kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ambapo mfanyakazi wa nyumbani, Anitha Gabriel aliyefuatilia madeni katika mshahara wake wa miaka minne, hatimaye amepata stahiki zake.
Anitha ambaye alikuwa akimdai mwajiri wake zaidi ya Shilingi laki saba, sehemu ya mshahara wake wote iliyokuwa imebakia, baada ya kufanya kazi za ndani Jijini Arusha, amesaidiwa na timu ya msaada wa kisheria ya Mama Samia ambayo imetia nanga kwa siku kumi katika manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza.
Mwenyekiti wa mtaa wa Bugogwa, Jagan Said na Mwenyekiti wa mtaa wa Igombe A, Mathias Mkono wameipongeza kampeni hiyo kwa kuwafikia wananchi wanyonge, wakiwasihi wananchi wenye changamoto mbalimbali kujitokeza kupaza sauti zao ili kupata haki zao.
Kwa upande wake Mratibu wa kampeni hiyo Manispaa ya Ilemela, Koku Mwanemile ameeleza walivyofanikisha kupatikana kwa haki ya binti huyo, na wamewataka wananchi wenye shida mbalimbali kujitokeza kupata haki kupitia Kampeni hiyo.