Latest Posts

MGOGORO WA ARDHI KATI YA WAKALA WA MBEGU NA WANANCHI NAMTUMBO KUTATULIWA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewatoa hofu wananchi kuhusu mgogoro wa ardhi unaohusisha Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), akisisitiza kuwa suala hilo linafanyiwa kazi na serikali.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Rwinga, Wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma, tarehe 26 Septemba 2024, Rais Samia amesema kuwa ASA imepewa jukumu maalum la kuzalisha mbegu bora za kilimo kwa ajili ya wakulima nchini.
“Kuna jambo la mgogoro wa ardhi kule Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), na lenyewe tunalijua na tunalifanyia kazi,” amesema Rais Samia.
Ameweka wazi kwamba ASA wapo kwa lengo la kuzalisha mbegu bora za mazao yanayolimwa nchini, na serikali imeshaanza hatua za kutoa ruzuku ya mbegu, kama ilivyofanya kwa mbolea. Rais Samia ameeleza kuwa ruzuku ya mbegu itawezesha kushusha bei ya mbegu, huku serikali ikibeba nusu ya gharama ili kuwasaidia wakulima.
Rais Samia pia ameonesha dhamira ya serikali ya kuhakikisha kuwa mbegu zinazozalishwa ni za ubora wa hali ya juu, akisema: “Tunataka kuleta mbegu zilizo bora, mbegu ambayo ikipandwa inaota.”
Ameweka wazi kuwa serikali haitakubali tena udanganyifu wa kuuza mahindi ya kawaida yaliyochovwa rangi kama mbegu.
“Tunataka kutoka huko,” ameongeza, akisisitiza kuwa serikali ina mpango wa kupanua mashamba ya mbegu nchini ili kuhakikisha uzalishaji wa mbegu bora unafanyika ndani ya nchi.
Rais Samia amefafanua kuwa kwa sasa Tanzania inatumia fedha za kigeni kuagiza mbegu kutoka nje, lakini lengo la serikali ni kuzalisha mbegu zote ndani ya nchi. Amewahimiza wananchi kuacha Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) wafanye kazi yao kwa ufanisi ili kuhakikisha Tanzania inajitosheleza kwa uzalishaji wa mbegu bora.
“Suala la mgogoro wa ardhi tutaufanyia kazi, lakini tunaomba sana waacheni ASA wafanye kazi yao watuzalishie mbegu,” amesema Rais Samia, akieleza dhamira ya serikali ya kuboresha sekta ya kilimo kwa kuhakikisha wakulima wanapata mbegu za uhakika, zenye ubora, na zinazochangia tija katika uzalishaji wa mazao.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!