Mila na desturi za zamani zimetajwa kuwa sababu kuu inayowafanya wanaume wengi kushindwa kushiriki kikamilifu katika afya ya uzazi wa wenza wao pamoja na watoto.
Wanaume wanahofia kuchekwa na kudharauliwa na jamii inayowazunguka, kwa kuzingatia kwamba masuala ya afya ya uzazi ni ya wanawake pekee, kulingana na desturi za Kiafrika.
Kutokana na hali hiyo, serikali imeanzisha mpango wa kuandaa mwongozo utakaosaidia kuwashirikisha wanaume zaidi katika afya ya uzazi. Mwongozo huu utawafanya wanaume kuwa sehemu ya mchakato wa kuwasaidia wenza wao kuhudhuria kliniki wakati wa ujauzito na kujifungua, hatua inayolenga kupunguza vifo vya mama na mtoto. Serikali inaamini kuwa ushiriki wa wanaume katika nyanja hii utaondoa changamoto ambazo zimekuwa zikiwazuia kushiriki kikamilifu.
Akizungumzia ujio wa program hiyo, Mratibu wa shirika la Tanzania Men as Equal Partners in Development (TMPid), John Komba, amesema kuwa kuna umuhimu wa wanaume kushiriki katika afya ya uzazi. Komba ameeleza kuwa wanaume wengi hawana taarifa za kutosha juu ya afya ya uzazi na wanadhani kuwa ni jukumu la wanawake pekee, jambo ambalo si sahihi.
“Mwanaume ana nafasi kubwa katika kuboresha matumizi ya huduma za afya ya uzazi tangu mimba inavyotungwa hadi wakati wa kujifungua. Mila na desturi zimekuwa kikwazo, lakini kwa elimu inayotolewa tunaamini itaweza kusaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto,” amesema Komba.
Kwa upande wake, Desteria Nanyanga, Afisa kutoka Wizara ya Afya, Idara ya Uzazi na Mtoto, amesema kuwa wizara hiyo imeandaa mwongozo ambao utatumika katika vituo vya huduma za afya ili kuwashirikisha wanaume kikamilifu katika kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Alisema, “Ili tuweze kufikia malengo ya kimataifa ya kupunguza vifo vya uzazi, tunahitaji mikakati kabambe, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba baba anamhamasisha mama kuhudhuria kliniki na kujifungulia katika vituo vya afya. Baba anapaswa kuelewa vizuri afya ya uzazi, ili aweze kuchangia kikamilifu kuboresha afya ya familia.”
Dk. Zabron Masatu, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, ameunga mkono mpango huo na kusema kuwa wanaume wengi hawashiriki katika masuala ya afya ya uzazi, jambo ambalo limekuwa kikwazo katika juhudi za kupunguza vifo vya uzazi.
Amehitimisha kwa kusema kuwa, kupitia programu hii mpya, wanaamini wanaume wakitambua majukumu yao katika afya ya uzazi, wataweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto zinazowakabili wanawake na watoto.