Latest Posts

MPOGOLO: SERIKALI IMEJIPANGA KUIMARISHA MAZINGIRA YA BIASHARA KARIAKOO

Katika kuhakikisha wafanyabiashara wa Soko Kuu la Kimataifa Kariakoo wanapata huduma bora na kufanya biashara katika mazingira rafiki, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema halmashauri hiyo ipo tayari kushirikiana na mamlaka mbalimbali, ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Mpogolo aliyasema hayo jijini Dar es Salaam, wakati wa mkutano uliowakutanisha viongozi wa halmashauri ya Ilala, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo.

Amesema halmashauri kwa kushirikiana na wafanyabiashara, wakiwemo wajasiriamali wadogo (machinga), imejipanga kuboresha mazingira ya biashara sokoni hapo ili kuwasaidia wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa ufanisi na kulipa kodi kwa urahisi. Amebainisha kuwa wafanyabiashara wanapokuwa katika mazingira bora ya biashara, wanakuwa tayari kulipa kodi kwa hiari kuliko wanavyofanya sasa, huku wengi wakilazimika kufanya biashara katika maeneo yasiyo rasmi kama barabarani.

Mpogolo pia amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kiasi cha Shilingi bilioni 28 kwa ajili ya ujenzi wa Soko Jipya la Kimataifa Kariakoo, kutokana na soko la awali kuungua moto. Pia amepongeza hatua ya serikali kugharamia ujenzi wa Soko la Jangwani, ambalo litawapokea wafanyabiashara wadogo.

Aidha, amemtaka Afisa Biashara wa Ilala kuandaa kanzidata (database) ya wafanyabiashara waliopo sasa Kariakoo, ili kuhakikisha wanapewa kipaumbele katika ugawaji wa nafasi mara baada ya kukamilika kwa soko jipya, na kuondoa changamoto za malalamiko ya kukosa maeneo ya biashara.

Mkuu huyo wa wilaya amemhakikishia Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, kwamba ofisi yake iko tayari kushirikiana na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo na Dar es Salaam kwa ujumla, kwa kutambua mchango wao mkubwa katika uchumi wa nchi kupitia ajira na ulipaji wa kodi.

Pia amewataka wafanyabiashara ambao bado hawajajiunga na umoja wowote wa wafanyabiashara kufanya hivyo, ili iwe rahisi kushughulikia changamoto zao kwa pamoja kupitia viongozi wao wa umoja huo.

Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa TRA, Yussuf Mwenda, amesisitiza kuwa soko la Kariakoo linazalisha walipa kodi wakubwa, wa kati na wadogo, na kwamba mamlaka hiyo inajivunia mchango wa wafanyabiashara wa eneo hilo katika kukuza uchumi wa taifa.

Ameeleza kuwa TRA imeandaa mipango mitatu muhimu kwa wafanyabiashara wa Kariakoo, ikiwemo kuhakikisha wazawa wanakuwa mabilionea kupitia biashara zao, badala ya kuona mabilionea wa Kariakoo wakiwa wageni pekee.

Wafanyabiashara wa Kariakoo, kwa upande wao, wamesema wako tayari kulipa kodi ili wafanye biashara zao kwa amani, huku TRA ikiahidi kugharamia utayarishaji wa kanzidata ya wafanyabiashara wa Kariakoo ili waweze kutambulika rasmi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!