Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, ametoa wito kwa waajiri na viongozi wa ofisi za umma kuwatumia Waandishi Waendesha Ofisi (Masekretari) katika kuandaa nyaraka rasmi kwa Kiswahili sanifu na fasaha badala ya kuandika wenyewe, hali inayosababisha makosa mengi kwenye nyaraka hizo.
Msigwa ametoa kauli hiyo mkoani Morogoro wakati akifunga mafunzo ya matumizi ya Kiswahili sanifu na fasaha kwa Masekretari yaliyoandaliwa na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA). Amesema viongozi wengi wanakabiliwa na majukumu mengi yanayowafanya kushindwa kuandika kwa usahihi na kusababisha nyaraka nyingi zenye makosa.
“Fanyeni utafiti, nyaraka nyingi zenye makosa ni zile ambazo maboss wamejifungia kuandika wenyewe. Wanaandika wakiwa na stress, wanakimbizana na muda, na matokeo yake ni nyaraka zenye makosa. Masekretari mnapaswa kuwaonesha tofauti kwa kutumia ujuzi wenu wa Kiswahili sanifu,” amesema Msigwa.
Katibu Mkuu amewahimiza viongozi kuwapa fursa Masekretari kushiriki mafunzo ya ndani na nje ya nchi kuhusu matumizi ya Kiswahili sanifu na fasaha ili kuboresha utendaji wao. Amesisitiza kuwa Masekretari wanapaswa kuwa msaada wa karibu kwa viongozi wao katika maandalizi ya taarifa na nyaraka za ofisi.
Aidha, Msigwa amesisitiza kuwa kampeni za matumizi ya Kiswahili sanifu ni sehemu muhimu ya kuboresha mawasiliano rasmi serikalini na kuhakikisha nyaraka zinakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.