Latest Posts

MTANDAO WA KUPINGA RUSHWA YA NGONO WAPINGA MAREKEBISHO YA SHERIA YA KUZUIA NA KUPAMBANA NA RUSHWA

Mtandao wa Kupinga Rushwa ya Ngono, unaojumuisha mashirika zaidi ya 200, umetoa tamko kali kupinga marekebisho yanayopendekezwa kwenye Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, hususan kifungu 10(b). Kwa mujibu wa mtandao huo, marekebisho hayo yanahatarisha juhudi za kupambana na rushwa ya ngono kwa kumlenga mwathirika badala ya kumwajibisha mhalifu.

Tamko hilo limetolewa na Mtandao wa Kupinga Rushwa ya Ngono siku ya Jumamosi Agosti 31, 2024 jijini Dar es Salaam, ukiongozwa na Rebeca Gyumi, mmoja wa wanaharakati wakubwa wa haki za wanawake nchini Tanzania.

Gyumi ambaye pia ni mkurugenzi wa shirika la Msichana Initiative, amesema kuwa marekebisho yanayopendekezwa katika kifungu 10(b) yanalenga kuhalalisha vitendo vya rushwa ya ngono kwa kutoa mwanya wa kisheria kwa wahalifu kujihami dhidi ya matendo yao.

“Kifungu hiki kinageuza hali halisi kwa kumfanya mwathirika wa rushwa ya ngono kuwa mhalifu badala ya kumlinda. Hii ni kinyume na mantiki ya kimaadili na kanuni za haki,” amesema Rebeca Gyumi.

Mtandao huo umesisitiza kuwa kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007 kinajitosheleza na hakihitaji marekebisho yoyote. Kwa mujibu wa mtandao huo, kifungu hiki kilitokana na utafiti na uzoefu wa majaji wanawake nchini Tanzania, ambao walitambua kuwa rushwa ya ngono inatokana na tofauti za kimamlaka kati ya mhalifu na mwathirika, na si suala la makubaliano kama ilivyo kwenye biashara ya ngono.

“Watu wenye mamlaka wanatarajiwa kujiendesha kwa uadilifu na kuwasaidia walio chini yao kushikilia viwango vya maadili. Mabadiliko haya yanawafanya waonekane kama viumbe dhaifu, wasioweza kuhimili vishawishi,” ameongeza Rebeca Gyumi.

Mtandao wa Kupinga Rushwa ya Ngono umewataka wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha muswada huu haupiti, kwani utavuruga juhudi za kuhakikisha haki inatendeka kwa waathirika wa rushwa ya ngono nchini.

Wanamtandao pia wamependekeza kwamba kifungu cha 10(b) kiondolewe na kifungu cha 25 kiendelee kutumika kama kilivyo, ili kuhakikisha kuwa sheria inawalinda waathirika na kuwawajibisha wahalifu bila mapendeleo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!