Latest Posts

MTOTO (09) AFARIKI DUNIA AKIDAIWA KUJINYONGA UYOLE JIJINI MBEYA

Na Josea Sinkala, Mbeya.

Simanzi na vilio vimetawala katika mtaa wa Mwanyanje kata ya Igawilo Uyole jijini Mbeya baada ya mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya msingi Iganjo kukutwa amefariki dunia katika mazingira yaliyoelezwa kuwa ya kujinyonga au kunyongwa.

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Oktoba 30, 2024 ambapo mwili wa mtoto huyo aliyetajwa kwa jina la Brighton Mbilinyi (09) umekutwa ukining’inia mahali mita chache kutoka nyumbani kwao.

Akizungumzia tukio hilo la simanzi, mama mzazi wa kijana huyo Bi. Tulinde Sanga ambaye ni mfanyabiashara ndogondogo, amesema Oktoba 29, 2024 mwanaye huyo mkubwa aliamshwa na kujiandaa kwenda shule lakini hakurudi na kuanza kumtafuta hadi alipokutwa amefariki dunia katika hali inayoonekana ya kujinyonga au kunyongwa na kutelekezwa katika mazingira hayo.

“Jana (Oktoba 29, 2024) nilimuamsha mwanangu (Marehemu Brighton Mbilinyi) ili ajiandae kwenda shuleni alijiandaa na akaondoka kwenda shule namimi nikaondoka kwenda kwenye biashara zangu lakini baadaye nilivyorudi nikakuta mtoto hajarudi ikafika saa moja usiku hajarudi tukaenda kumpa taarifa balozi tukashauriana kwenda kutoa taarifa Polisi na majirani zangu wakasema akipatikana tuwape taarifa lakini leo (Oktoba 30, 2024) kumekucha ndio majirani wakasema njoo uangalie huku ndipo tukakuta mwili wake kwenye lile pagala kwakweli ninasikitika na mwanangu hakuwa na tatizo lolote”, ameeleza mama mzazi wa marehemu Brighton Mbilinyi.

Wananchi katika mtaa wa Mwanyanje wameeleza kusikitishwa na tukio hilo na kuwaomba wananchi wenzao kuwa karibu na watoto wao ikiwa ni pamoja na kufuatilia mienendo yao shuleni.

Balozi wa eneo hilo Madawa Mwamboneke, amesema baada ya taarifa hizo kuarifiwa aliwajulisha ofisi ya afisa mtendaji wa mtaa wa Mwanyanje na Polisi ambapo muda mfupi baadaye Polisi walifika na kuchukua mwili wa marehemu ambao umehifadhiwa katika hospitali ya wilaya Igawilo kwa ajili ya taratibu za kiuchunguzi kisha baadaye taratibu za maziko.

Alipoulizwa kuhusu tukio hilo kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Benjamin Kuzaga, amesema alikuwa nje ya ofisi kwa majukumu ya kikazi hivyo kuahidi kufuatilia tukio hilo ili kupata taarifa kamili kutoka kwa msaidizi wake.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!