Viongozi waandamizi 37 kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) wamepiga kambi kwa siku tatu katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere Kibaha, kwa ajili ya mafunzo maalum ya uongozi bora yenye lengo la kuimarisha utendaji na kuleta ufanisi katika taasisi hiyo ya elimu ya juu ya tiba.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Apolinari Kamuhabwa, alisema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwajengea viongozi wa chuo hicho uelewa wa pamoja katika masuala ya uendeshaji wa taasisi, usimamizi wa rasilimali, na utekelezaji wa miradi ya kimkakati kwa ufanisi.
“Tumeomba mafunzo haya kwa hiari kwa kuchagua kozi zinazotuhusu — uongozi wa watu, usimamizi wa fedha na miradi, uzalendo, na namna bora ya kutatua changamoto zinazojitokeza katika uendeshaji wa taasisi,” alisema Prof. Kamuhabwa.
Amesisitiza kuwa MUHAS ni taasisi yenye wajibu mkubwa kwa jamii, hivyo ni lazima viongozi wake wawe na uelewa wa pamoja na uwezo wa kisasa wa uendeshaji wa taasisi zinazohusika na afya na maendeleo ya binadamu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Simon, akifungua rasmi mafunzo hayo, alisisitiza juu ya umuhimu wa unyenyekevu katika uongozi na kuwahimiza viongozi kuwasikiliza wale wanaowaongoza.
“Cheo si sababu ya kujitenga na jamii. Kiongozi ni mtumishi wa watu, hivyo tambueni thamani ya kila mmoja na kuonyesha utu katika kila hatua,” alisema DC Simon.
Ameongeza kuwa viongozi wa afya, hasa madaktari, wanapaswa kuwa na moyo wa kusikiliza wagonjwa kwa uvumilivu na upendo, kwani mazingira ya hospitali huambatana na changamoto nyingi kwa wananchi.
Awali, Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Prof. Marceline Chijoriga, alisema kuwa kozi hiyo ni ya 66 tangu kuanzishwa kwa shule hiyo, na hadi sasa zaidi ya washiriki 14,000 kutoka taasisi mbalimbali nchini wameshapata mafunzo ya uongozi bora.
“Tunasisitiza nidhamu, uzalendo, na uongozi wa kizalendo unaojali faida kwa taifa. Viongozi wanaopitia hapa wanakuwa chachu ya mabadiliko serikalini na katika jamii,” alisema Prof. Chijoriga.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wazazi kutowapa vijana uhuru usio na mipaka, akieleza kuwa wao ndio viongozi wa baadaye wanaopaswa kulelewa katika misingi ya maadili na nidhamu ya kazi.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuendelea kwa awamu nyingine zitakazolenga wakuu wa idara, vitengo, na watumishi wote wa MUHAS kama sehemu ya mpango endelevu wa kujenga uwezo na kuleta matokeo chanya katika sekta ya elimu ya juu ya afya nchini.