Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia kwa Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, imekanusha vikali tuhuma za utesaji na unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanaharakati wawili kutoka Kenya na Uganda-Boniface Mwangi na Agather Atuhaire.
Kamanda Muliro ameiambia BBC kuwa iwapo wanaharakati hao waliteswa walipokuwa Tanzania, basi walipaswa kutoa malalamiko rasmi katika mamlaka husika kwa ajili ya uchunguzi. Amesisitiza kuwa madai yao, yanayodaiwa kutolewa nje ya mfumo rasmi wa sheria, ni maoni yasiyofaa kuchukuliwa kama ushahidi wa moja kwa moja.

“Kama wangekuwa hapa, ningewashirikisha, ningewauliza wanasema nini, wanamaanisha nini… Katika sheria, mambo hayo yanaitwa ushahidi wa tetesi au tetesi,” amesema Muliro.
Akizungumza na DW Kiswahili, Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa alisema madai ya unyanyasaji huo hayana msingi wowote na yana lengo la kuichafua sura ya Tanzania kimataifa.
“Hii nchi ina heshima zake, inaheshimiwa na kila mtu na watu wote wanaifahamu Tanzania, wao si watu wa kwanza kuja Tanzania, watu wengi wamekuja Tanzania. Kama wao wanakwenda kuzalisha tuhuma zao za uongo, wacha waendelee kufanya lakini Tanzania haiko hivyo. Wao walivunja sheria, wamechukuliwa hatua,” alisema Msigwa.
Aliongeza kuwa wanaharakati hao walivunja sheria za nchi na kuchukuliwa hatua kulingana na taratibu, na alitahadharisha dhidi ya watu wanaotaka kulazimisha siasa na tamaduni za nje nchini Tanzania.
Kundi la mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Kenya, likishirikiana na Chama cha Mawakili wa Kenya (LSK), limeitaka Jumuiya ya Kimataifa na Jumuiya ya Afrika Mashariki kuishinikiza Tanzania kuwachukulia hatua maafisa wote wanaodaiwa kuhusika na mateso dhidi ya Mwangi na Atuhaire.
Katika mkutano na waandishi wa habari jijini Nairobi, wanaharakati hao walidai kuwa wakiwa chini ya mamlaka ya polisi wa Tanzania, walipigwa, kunyanyaswa na hata kubakwa kabla ya kurejeshwa katika nchi zao.