Latest Posts

MVUTANO WA KISIASA: BURUNDI YATISHIA KUJIBU VIKALI UVAMIZI WOWOTE KUTOKA RWANDA

Burundi imeonya kuwa itajibu kwa nguvu zote iwapo Rwanda itaishambulia kwa njia yoyote ile, huku Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye, akidai kuwa taifa jirani la Rwanda linapanga kuivamia kupitia ardhi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Akizungumza na Kituo cha habari cha BBC hivi karibuni, Rais Ndayishimiye amesema wamepata taarifa za kuaminika kuwa Rwanda inajaribu kuishambulia Burundi kwa kutumia waasi wa Red Tabara na M23 kama kisingizio.

“Tunafahamu Rwanda inajaribu kutuvamia kupitia ardhi ya DRC ili wasingizie waasi wa Red Tabara na M23. Lakini tunawaambia kwamba ikiwa mnaona kushambulia Bujumbura ni karibu kutoka Uvira basi nasi tunaweza kushambulia Kigali kutoka mji wa Kirundo,” ameonya Rais Ndayishimiye.

Hata hivyo, Rwanda imekanusha madai hayo, huku msemaji wa serikali yake, Yolanda Makolo, akisema matamshi ya Burundi yanashangaza kwa kuwa mataifa hayo mawili yamekuwa na mazungumzo ya mara kwa mara kuhusu usalama wa mpaka wao.

Burundi imesema tayari imepeleka ujumbe rasmi kwa Rais wa Rwanda, Paul Kagame, kuhusu haja ya kutekeleza makubaliano ya maridhiano ili kupunguza uhasama kati ya mataifa hayo mawili.

“Tumefanya mazungumzo na Rwanda kwa muda mrefu na tukakubaliana, lakini ilipofika wakati wa utekelezaji, Rwanda ikasita,” amesema Rais Ndayishimiye.

Burundi pia imeishutumu Rwanda kwa kuwapa hifadhi watu wanaoaminika kuwa walihusika katika jaribio la mapinduzi ya serikali ya Burundi mwaka 2015 na pia kwa kufadhili waasi wa Red Tabara wanaofanya mashambulizi kutoka Mashariki mwa DRC.

Katika hatua nyingine, Burundi imefunga mipaka yake na Rwanda kutokana na mashambulizi ya hivi karibuni yanayodaiwa kufanywa na waasi wa Red Tabara. Serikali ya Burundi imesisitiza kuwa haitaweka mezani mazungumzo yoyote na waasi hao na badala yake itaendelea kuwawinda na kuwafikisha mahakamani.

Rais Ndayishimiye amehitimisha kwa kusema kuwa Burundi haina nia ya kuvamia nchi nyingine au kuingilia masuala ya ndani ya mataifa mengine, na hivyo inastahili kupewa heshima kama hiyo pia.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!