Collins Leitich Chepkulei, mwanaume aliyegonga vichwa vya habari kwa kuanzisha kituo cha polisi kisicho na idhini katika Kituo cha Cherus, Kaunti ndogo ya Kesses jijini Nairobi nchini Kenya, sasa anasema kuwa kituo hicho kilikuwa kimekuwepo kwa siku tano pekee na hakukuwa na maafisa wa polisi waliokuwa wametumwa kufanya kazi hapo.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumanne, Leitich amekana madai kwamba alikuwa akijifanya afisa wa polisi, akisema vyombo vya habari vimeeneza taarifa zisizo sahihi.
“Sijawahi kujifanya polisi, wala hatujawaweka polisi kwenye kituo hicho. Kituo hicho ni kipya tu, ni cha siku tano pekee, hata rangi bado haijakauka,” amesema Leitich.
Kwa mujibu wa Leitich akirejelewa na chombo cha habari cha Citizen Digital, uamuzi wa kuanzisha kituo hicho ulitokana na matukio ya mara kwa mara ya ukosefu wa usalama katika eneo hilo.
Amesema wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa uwepo wa polisi kwa muda mrefu, huku kituo cha polisi kilicho karibu kikiwa kilomita saba kutoka kijijini.
“Niliamua kupaka rangi jengo hilo kwa msaada wa jamii… si kwa matakwa yangu binafsi bali kwa niaba ya jamii nzima. Hii ni kwa sababu ya changamoto za usalama zinazotukumba,” amefafanua.
Leitich ameongeza kuwa, kwa kuwa serikali haikuwa imeanzisha kituo cha doria katika eneo hilo, wakazi waliamua kuchukua hatua wenyewe na kuchangisha fedha ili kuleta huduma za usalama karibu nao.
“Kama jamii, tumekuwa na changamoto za usalama na tumekuwa tukiomba serikali itupe kituo cha polisi kwa muda mrefu. Hatulaumu mamlaka kwa sababu huenda hakuna fedha, hivyo basi tukajiuliza kwa nini tusikusanye pesa wenyewe? Mimi nikawa mfadhili mkuu wa mradi huu ili kuleta huduma za polisi karibu nasi,” amesema.
Ili kuthibitisha kuwa hakuchukua uamuzi huo peke yake, Leitich amesema alifanya mashauriano na viongozi wa eneo hilo, wakiwemo wawakilishi wa Nyumba Kumi, kabla ya kuanza mradi huo.
“Nina uungwaji mkono wa jamii kwa sababu tulikuwa pamoja kwenye jambo hili. Nilizungumza na viongozi wa Nyumba Kumi kabla ya kuanza mradi huu. Sitaki kutaja majina, lakini tulifanya kikao,” amesema.
Leitich amekiri kuwa huenda hakufuata taratibu zote sahihi katika kuanzisha kituo hicho, lakini ameahidi kurekebisha kasoro zilizojitokeza ili mradi huo uwe halali.
“Kuna taratibu za kufuata. Siwezi kusema kama nilifanya kosa au la, lakini kabla ya kupaka rangi na kuanzisha kituo, lazima uwe umepitia hatua fulani. Huenda hatukukamilisha hatua zote, lakini tulianza kwa baadhi ya hatua,” ameeleza.
Ameongeza kuwa yuko tayari kushirikiana na mamlaka kuhakikisha kuwa kituo hicho kinakuwa halali, huku akiomba radhi kwa serikali ikiwa wamekosea.
“Tunarekebisha makosa yetu ili kituo kiwe halali. Kama tumekosea serikali, tunaomba msamaha. Labda hatukufuata taratibu zote, lakini kuanzia sasa tutakuwa makini zaidi na kufuata sheria,” amesema Leitich.