Latest Posts

MWIGULU AAHIDI KUSAIDIA WATOTO WA MTUMISHI WA TRA, ALAANI VIKALI MAUAJI YAKE

Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu, ameahidi kuwahudumia kimahitaji watoto wawili wa marehemu, Amani Kamguna Simbayao, aliyekuwa mtumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), aliyefariki dunia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kutokana na kushambuliwa na watu katika eneo la Tegeta kwa Ndevu, mkoani Dar es Salaam, tarehe 6 Disemba, 2024.

Dkt. Nchemba ametoa ahadi hiyo wakati akiongoza waombolezaji kuuaga mwili wa marehemu katika Viwanja vya Michezo vya TRA, Kurasini, Dar es Salaam.

Aidha, Dkt. Nchemba, amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, ambaye aliwakilishwa na Naibu Katibu Mkuu, Bw. Elijah Mwandumbya, katika tukio hilo, na Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuf Juma Mwenda, kuhakikisha kuwa kiasi cha Shilingi milioni 200 kinatafutwa kwa ajili ya kuanzisha mfuko maalum utakaotumika kuwanunulia watoto hao (Najimu Amani Sumbayao (8) na Badria Amani Simbayao (3), pamoja na mama yao, Bi. Arafat Abdalla Ukomo, Hati Fungani za Benki Kuu ya Tanzania, kwa ajili ya uhakika wa kupata huduma stahiki kama vile elimu na mambo mengine.

Maelekezo hayo yanafuatia maombi yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, wakati akitoa salam za mkoa wake, ambapo alipendekeza uwepo wa mpango mahsusi wa kuisaidia familia hiyo kimaisha ili iwe motisha kwa familia hiyo iliyopoteza shujaa aliyemwaga damu yake wakati akilitumikia Taifa.

Marehemu Amani Simbayao, alikuwa Afisa Usafirishaji (dereva) wa TRA, alifariki baada ya kupigwa na kuumizwa vibaya na watu akiwa kazini, na wafanyakazi wenzake wengine wawili wakati walipokuwa wakilifuatilia gari moja lililokuwa linashukiwa kukiuka masuala ya kiforodha.

Katika tukio hilo la kuuaga mwili wa marehemu, Dkt. Nchemba, alilaani vikali tukio hilo la watu kujichukulia sheria mkononi na kumuua mtumishi asiye na hatia hata baada ya kujitambulisha kuwa ni mtumishi wa TRA, na ametoa wito kwa vyombo vya dola kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote waliohusika na tukio hilo ili liwe fundisho kwa watu wengine.

Aliwatia moyo wafanyakazi wa TRA, wasikatishwe tamaa na tukio hilo, bali waendelee kuchapakazi kwa bidii kwa manufaa ya taifa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!