Latest Posts

PM MAJALIWA: TUNATAKA MAJI YA MVUA YASIPOTEE TENA, YATUMIKE KWA MAENDELEO

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, amesema Serikali imejipanga kikamilifu kuyatumia mabonde ya mito nchini kama njia ya kudhibiti athari za mafuriko na kuboresha huduma za kijamii kama maji, umeme, kilimo na mifugo.

Amesema hayo Alhamisi, Aprili 24, 2025 wakati akijibu swali la mbunge wa Kyela, Ally Anyigugile Jumbe aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kukabiliana na mafuriko nchini, wakati wa kipindi cha Maswali ya Wabunge kwa Waziri Mkuu.

Amesema moja ya hatua muhimu ni kuanzisha mamlaka za mabonde zitakazoratibu matumizi na ufuatiliaji wa rasilimali za maji ili kuhakikisha zinawanufaisha Watanzania kwa namna endelevu.

“Kama ilivyo kwa Bonde la Rufiji, tumeanzisha mradi mkubwa wa kuzalisha umeme. Pia Morogoro kuna ujenzi wa bwawa kubwa litakalotumia maji ya Mto Ruvu kwa ajili ya maendeleo ya taifa,” amesema Waziri Mkuu.

Majaliwa ameeleza kuwa Serikali imejipanga kuongeza bajeti kwa Wizara ya Kilimo, Maji na Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) ili kuhakikisha maji ya mvua yanatumika badala ya kuleta madhara.

“Tunalenga kuhakikisha maji hayapotei bure. Badala yake yatatumika kwa kilimo, nishati, na huduma za jamii,” amesisitiza.

Katika kujibu swali la Mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Tarimo, kuhusu tofauti ya mishahara kwa watumishi wa kada zinazofanana, Waziri Mkuu amesema Serikali tayari imeanzisha idara maalum inayoratibu mishahara, posho na marupurupu, huku ikifanya mapitio ya kila mwaka kuhakikisha yanakwenda sambamba na hali ya uchumi wa taifa.

Waziri Mkuu ameeleza kuwa Serikali imeanzisha wizara maalum kwa ajili ya masuala ya kijamii inayosimamia mapambano dhidi ya ukatili, ikishirikiana na wadau wa maendeleo, taasisi za elimu na vyombo vya ulinzi na usalama.

“Tumeanzisha madawati ya jinsia katika shule, vyuo na taasisi za ulinzi. Lakini pia kila Mtanzania anapaswa kuwa mlinzi wa haki za binadamu katika jamii yake,” amesema Waziri Mkuu.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!