Latest Posts

POLISI WAANZA UCHUNGUZI WA KIFO CHA MWANAMKE WA MIAKA 19 AKIWA NYUMBANI KWA MPENZI WAKE

Maafisa wa uchunguzi wa jinai (DCI) katika Kituo cha Polisi cha Lang’ata, Nairobi nchini Kenya wanafanya uchunguzi kuhusu mazingira ya kifo cha mwanafunzi mhitimu wa Kidato cha Nne mwenye umri wa miaka 19, aliyefariki kwa hali isiyoeleweka akiwa katika sherehe ya siku yake ya kuzaliwa nyumbani kwa mpenzi wake.
 
Kwa mujibu wa polisi, wamepokea taarifa kuhusu kifo hicho kutoka kwa nyumba moja eneo la Mbagathi, lakini hakukuwa na ushahidi wa wazi wa kutambua chanzo chake.
 
Wapelelezi sasa wanategemea vipimo vya sumu (toxicology tests) ili kubaini kiini cha kifo cha mwanafunzi huyo, ambaye kwa sasa ametajwa kama Faith.
 
Faith aliondoka nyumbani kwa wazazi wake kusheherekea siku yake ya kuzaliwa na marafiki zake. Wakiwa watu watano, walielekea kwenye kituo maarufu cha burudani kando ya Barabara ya Lang’ata, ambako walifurahia sherehe yao.
 
Baada ya muda, kundi hilo lilitawanyika, na Faith akaamua kwenda nyumbani kwa mpenzi wake akiwa na rafiki yake wa kike mmoja. Ilipofika saa sita za usiku, rafiki yake aliondoka, akimuacha Faith peke yake nyumbani kwa mpenzi wake.
 
“Sisi tulikuwa tu hapo tukifurahia, tukibadilishana stori. Baadaye Mark akasema anaenda kulala, akatuambia sisi tulale kwa kiti. Kidogo mamangu akanifuata, nikatoka…” alisema rafiki wa Faith, ambaye jina lake halikutajwa.
 
Kesho yake, rafiki yake alijaribu kumpigia simu Faith bila mafanikio. Ilipofika saa 11 jioni (5 p.m.), alipokea simu isiyo ya kawaida kutoka kwa mpenzi wa Faith, aliyemjulisha kuwa Faith alikuwa amefariki dunia.
 
“Sasa yeye (mpenzi wa Faith) alienda kazini akarudi saa 11 jioni. Tulikutana naye kwenye ngazi, akaniuliza kama nina funguo. Nyumba ilikuwa imefungwa. Ghafla akapata funguo nyingine ya akiba na akaifungua. Kufungua, akaniita akasema Faith yuko kitandani amekufa. Nilipoenda nikamgusa, niligundua alikuwa tayari amefariki,” alisimulia shahidi mmoja.
 
Habari hizo zilimchanganya kila mtu, huku baba yake Faith, Momanyi Atisa, akishikwa na mshtuko alipofika eneo la tukio.
 
“Nilipofika, nilikuta watu wamejaa. Nilichanganyikiwa kabisa kusikia kuwa Faith amekufa. Nilizirai. Tulipeleka mwili hadi Mbagathi, tukaukuta tayari ukiwa kwenye meza,” alisema kwa uchungu.
 
Momanyi alisema alijitahidi kumlea Faith na kuhakikisha anapata elimu bora kwa matumaini ya maisha mazuri ya baadaye.
 
Baada ya kupata alama ya B katika mtihani wake wa Kidato cha Nne, Faith alikuwa anatarajiwa kujiunga na chuo kikuu mwaka huu.
 
“Alikuwa tayari kuendelea mbele. Alikuwa tegemeo langu. Nilihangaika kuhakikisha anasoma, lakini sasa ametutoka ghafla,” amesema kwa uchungu.
 
Uchunguzi wa mwili wake ulibaini kuwa Faith alikosa hewa na kwamba kulikuwa na maji mengi kwenye mapafu yake. Wapelelezi wamechukua sampuli zaidi kwa uchunguzi wa sumu katika maabara ya serikali, kabla ya kuchukua hatua zaidi.
 
Mpenzi wa Faith kwa sasa anashikiliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi kuhusu mazingira ya kifo chake.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!