Latest Posts

RAIS RUTO: MASLAHI YA NJE YANAENDELEZA MACHAFUKO DRC

Rais wa Kenya na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dkt. William Ruto, ameonya kuwa mgogoro unaoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) hauchochewi tu na matatizo ya ndani, bali pia na masilahi ya nje yanayoendeleza hali ya machafuko kwa faida za kiuchumi na kisiasa.

Akihutubia Mkutano wa Pamoja wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa EAC na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) jijini Dar es Salaam, Rais Ruto amesema kuwa juhudi za kikanda za kuleta amani lazima zizingatie pia ushawishi wa nje ambao umekuwa kikwazo kwa utulivu wa DRC.

“Ni wazi kwamba mgogoro huu wa DRC si suala la ndani pekee. Kuna mikono ya nje inayochochea vita kwa masilahi binafsi, ikihusisha unyonyaji wa rasilimali, siasa za kikanda, na hata njama za kiuchumi zinazoendelea kwa miongo kadhaa. Ni lazima tukatae hali hii na kusimama kwa umoja kuutafutia suluhisho la kudumu,” amesema Rais Ruto.

Amesisitiza kuwa hali ya ukosefu wa utulivu nchini DRC inafifisha juhudi za maendeleo barani Afrika na kudhoofisha mshikamano wa kikanda.

“Tunaposhuhudia vurugu zinazoendelea Mashariki mwa DRC, tunapaswa pia kujiuliza ni nani anayenufaika na hali hii? Wananchi wa Kongo wamechoshwa na vita, wanataka amani na maendeleo. Ni jukumu letu kuhakikisha tunasimama pamoja ili kuhakikisha amani inarejea kwao,” ameongeza.

Rais Ruto ametoa wito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuunga mkono juhudi za kidiplomasia badala ya kuruhusu masilahi binafsi kuendeleza hali ya machafuko.

“Tunazitaka pande zote katika mgogoro huu, hasa waasi wa M23, kuacha mara moja kusonga mbele na pia Jeshi la DRC kutochukua hatua za kulipiza kisasi. Amani ya kudumu haiwezi kupatikana kwa njia ya vita, bali kwa njia ya mazungumzo,” amesisitiza.

Kwa mujibu wa Rais Ruto, suluhisho la kudumu linapaswa kujikita katika mazungumzo ya kina yatakayohusisha wadau wote muhimu na kushughulikia mizizi ya mgogoro badala ya hatua za kijeshi zisizo na suluhisho la muda mrefu.

“Tusidanganyike kwamba tunaweza kutumia nguvu za kijeshi kuumaliza mgogoro huu. Lazima tukubali kwamba suluhisho pekee la kudumu ni diplomasia na mazungumzo yatakayohakikisha uhuru na mamlaka ya DRC yanaheshimiwa, huku wananchi wake wakihusishwa katika kuamua hatma yao,” amesema.

Akieleza hali ya kibinadamu inayoendelea kuzorota mashariki mwa DRC, Rais Ruto amesema kuwa maelfu ya watu wamepoteza maisha, mamilioni wamelazimika kuhama makazi yao, huku wanawake na watoto wakiendelea kuwa wahanga wa ukatili wa kijinsia na kuandikishwa jeshini kwa lazima.

“Ni aibu kwa dunia kuona mateso haya yakiendelea. Mamilioni ya watu wamepoteza makazi yao, na wengi wao wako katika hatari ya kufanyiwa ukatili wa kila aina. Jumuiya ya kimataifa inapaswa kuamka na kuchukua hatua za dhati kumaliza hali hii,” amesema.

Ametoa wito kwa mataifa ya nje kuepuka kuendeleza masilahi binafsi katika mgogoro wa DRC na badala yake kusaidia juhudi za amani.

“Ni wazi kuwa hali ya DRC inahusisha siasa za kimataifa. Tunatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuungana nasi katika juhudi za kuleta amani badala ya kuendeleza ajenda za kando ambazo zinaifanya DRC kuendelea kuwa uwanja wa vita vya milele,” ameongeza.

Kwa mara ya kwanza, jumuiya za EAC na SADC zimekutana kwa pamoja kujadili mustakabali wa DRC, hatua ambayo Rais Ruto alisema ni ishara ya umuhimu wa changamoto wanayokabiliana nayo na uthabiti wao katika kusaka suluhisho.

“Mkutano huu ni wa kihistoria kwa sababu kwa mara ya kwanza, jumuiya mbili za kikanda zinakutana kama ishara ya uzito wa changamoto tuliyonayo na dhamira yetu ya kuleta suluhisho. Lazima tuendeleze mshikamano huu na kuhakikisha tunapata suluhisho la kudumu,” amesema.

Amehimiza viongozi wa ukanda wa Afrika kuonesha mshikamano wa kisiasa na kujitoa kwa dhati katika kuhakikisha mgogoro huu unatatuliwa mara moja.

“Tunapaswa kuweka kando tofauti zetu, kuungana kwa nguvu zote, na kuhakikisha kuwa mgogoro huu unamalizika mara moja na milele. Historia itatuhukumu vikali tukikaa kimya na kuangalia hali inavyozidi kuwa mbaya,” alihitimisha Rais Ruto.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!