Latest Posts

RC SHIGELA: MSIRUDISHE WANAFUNZI NYUMBANI KWA SABABU YA MICHANGO

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martine Shigela, amepiga marufuku vitendo vya kuwarudisha wanafunzi nyumbani kwa sababu ya michango inayokubaliwa na wazazi katika ngazi ya kijiji au kitongoji, akisisitiza kuwa haki ya mtoto kupata elimu ni ya msingi na haihusishwi na suala la michango.

Akizungumza katika ziara ya siku moja katika kata za Nyamigota na Nyamwilolelwa, Mhe. Shigela alisema kuwa michango yoyote ile lazima ipitishwe kwa makubaliano ya wazazi bila kuathiri haki ya mtoto kupata elimu. Aliongeza kuwa shule hazipaswi kutumia michango kama kigezo cha kuwazuia watoto kuhudhuria masomo.

Katika kata ya Nyakagomba, Mkuu huyo wa Mkoa alitembelea na kukagua bwalo la chakula la Shule ya Sekondari Butundwe, ambalo limekamilika na kuanza kutumika. Mradi huo umegharimu zaidi ya shilingi milioni 366 kupitia mpango wa Uwajibikaji wa Makampuni kwa Jamii (CSR) kwa mwaka wa fedha 2021/2022. Mhandisi wa Halmashauri, Bi. Beatrice Mwaitete, alisema bwalo hilo litaleta tija kwa wanafunzi kwa kuwawezesha kula katika mazingira bora na kuokoa muda wa masomo.

Aidha, Mhe. Shigela alifanya mikutano ya hadhara katika kijiji cha CCM (kata ya Nyakagomba) na Saragulwa (kata ya Nyamwilolelwa), sambamba na ukaguzi wa ujenzi wa ofisi ya kata ya Nyamwilolelwa, unaogharimu zaidi ya shilingi milioni 94 kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri.

Akizungumzia maendeleo katika mkoa huo, Mhe. Shigela alisifu jitihada za kata ya Nyakagomba katika upandaji miti na maendeleo ya mtu mmoja mmoja. “Nimejionea maendeleo ya kweli kwa watu binafsi; nyumba nzuri na miti iliyopandwa ni viashiria vya maendeleo,” alisema.

Kwa upande wake, Diwani wa kata ya Nyamigota na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Mhe. Khadija Saidi, aliipongeza serikali kwa dhamira yake ya kuendelea kukamilisha miradi ya maendeleo kwa kushirikiana na viongozi wa maeneo husika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Ndg. Karia Magaro, alibainisha kuwa ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, miradi yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 59 imetekelezwa katika sekta za afya, elimu na miundombinu.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Sophia Jongo, alisema kuwa matukio ya wizi wa mifugo yamepungua kwa kiasi kikubwa kufuatia uanzishwaji wa vikundi vya ulinzi shirikishi. Hata hivyo, alikemea vikali vitendo vya ushirikina, hususan kwa waganga wa kienyeji wanaopiga ramli chonganishi na kutumia viungo vya binadamu, akisisitiza kuwa ni uhalifu wa jinai na hautavumiliwa.

Katika ziara hiyo, Mhe. Shigela pia alisikiliza kero mbalimbali za wananchi zikiwemo changamoto za maji, miundombinu na ongezeko la mbwa wa mitaani, ambapo alitoa maelekezo kwa mamlaka husika kuchukua hatua za haraka.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!