Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani ni fursa muhimu ya kuimarisha mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi kwa kuhamasisha jamii kushiriki katika kuzuia maambukizi, kudhibiti ugonjwa huo na kuunga mkono juhudi za kuutokomeza.
Akizungumza na waandishi wa habari Novemba 25,2026 jijini Dodoma kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya mwaka huu, Senyamule amesema siku hiyo huadhimishwa Desemba Mosi kila mwaka kwa lengo la kuwakumbuka watu waliopoteza maisha kutokana na Ukimwi, kuwaenzi wanaoishi na VVU pamoja na kutathmini hali na mwelekeo wa mapambano dhidi ya ugonjwa huo nchini na duniani.

Amesema maadhimisho hayo pia yanalenga kuhamasisha jamii kuendelea kushiriki katika ajenda ya kudhibiti Ukimwi, kutafakari mafanikio na changamoto zilizopo na kuimarisha mikakati ya kukabiliana na maambukizi ya VVU.
Ameeleza kuwa mwaka huu Mkoa wa Dodoma umepewa nafasi ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo kitaifa, ambayo kilele chake kitafanyika Desemba Mosi, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Dkt. Jakaya Kikwete (JKCC), huku Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Aidha, amesema kuelekea kilele hicho kutakuwa na maonyesho ya wadau wa mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi kuanzia Novemba 24 hadi Desemba Mosi, 2026 katika viwanja vya JKCC, ambapo wananchi watapata elimu na huduma mbalimbali ikiwemo ushauri nasaha na upimaji wa hiari wa VVU.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Huduma bora za afya ni msingi wa kutokomeza Ukimwi.”