Latest Posts

MTANZANIA AWEKEZA BILIONI 650+ KIWANDA CHA KLINKA ZA SARUJI KENYA, RAIS RUTO AMPONGEZA

Rais wa Kenya William Ruto amepongeza uwekezaji wa Shilingi za Kenya bilioni 32 (Zaidi ya Shilingi bilioni 650 za Kitanzania) wa kiwanda kipya cha kuzalisha klinka cha Bamburi Cement kilichopo Matuga, Kaunti ya Kwale akibainisha kuwa mradi huo ni hatua kubwa ya kuimarisha uzalishaji wa viwanda vya ndani na kupunguza utegemezi wa nchi kwa malighafi kutoka nje.

Akizungumza wakati wa sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi mnamo Novemba 24, 2026, Rais Ruto aliutaja uwekezaji huo kama mfano wa uwazi wa sera za serikali ya Kenya zenye lengo la kukuza viwanda nchini.

“Kwa kuchanganya uwepo mpana wa Bamburi Cement katika soko la ndani na uzoefu wake wa kioperesheni pamoja na utaalamu wa kiteknolojia wa kimataifa wa SINOMA- CBMI katika uhandisi na ujenzi wa viwanda vya saruji, ushirikiano huu utaimarisha kwa kiasi kikubwa uwezo wa uzalishaji wa klinka nchini, kupunguza utegemezi wa uagizaji nje, na kuongeza ushindani na ustahimilivu wa sekta ya saruji nchini Kenya”, alieleza Rais Ruto.

Kiwanda hicho kipya cha Matuga kinamilikiwa na kampuni ya Bamburi Cement, ambayo ilichukuliwa na kundi la kiviwanda la Amsons Group kutoka Tanzania mwaka 2024. Mradi huo unatarajiwa kuzalisha tani milioni 1.6 za klinka kwa mwaka (sawa na tani 5,000 kwa siku). Uwekezaji huu utaongeza uwezo wa Bamburi wa kuzalisha klinka kutoka tani milioni moja hadi tani milioni 2.6 kwa mwaka, huku uwezo wa jumla wa uzalishaji wa saruji ukiongezeka kutoka tani milioni 1.8 hadi tani milioni nne kwa mwaka. Hatua hii inalenga kuimarisha usambazaji wa malighafi inayohitajika kwa ajili ya miradi mikubwa ya miundombinu nchini.

Akizungumzia uwekezaji huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Amsons Group, Mtanzania Edha Nahdi alisisitiza uaminifu wa kundi hilo kwa uchumi wa Kenya akisema, “Kwa Amsons Group na Bamburi Cement… uwekezaji huu wa Dola milioni 250 ni kauli ya uaminifu wetu wa muda mrefu katika matarajio ya kiuchumi ya Kenya na dhamira yake ya kupanua viwanda vya ndani”.

Nahdi aliongeza kuwa Amsons Group iko tayari kuunga mkono mipango ya miundombinu ya serikali ikiwamo mpango kazi wa miaka 10 wa Rais Ruto wa uendelezaji na upanuzi wa miundombinu ya barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege, na mabomba ya mafuta.

“Kwa kutia saini mkataba huu wa EPC wa kukuza Kiwanda cha Klinka, Amsons Group inaweka fedha zake pale ilipo ahadi yake, ili kuwezesha maendeleo ya kitaifa na mabadiliko ya kiuchumi nchini Kenya”, alieleza Nahdi.

Malighafi ya klinka ambayo hutengenezwa kwa kuchoma mawe ya chokaa katika viwango vya juu vya joto kabla ya kusagwa na kujumuishwa na nyongeza zingine kutengeneza saruji ndiyo kiungo kikuu kinachotoa nguvu katika saruji.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bamburi Cement, Geoffrey Ndugwa, alieleza umuhimu wa kimkakati wa kiwanda hicho cha Kwale akisema, “Kiwanda hiki kipya cha Bamburi Matuga Clinker kinarudisha moyo huo nyumbani. Kitasaidia kulinda watengenezaji wa ndani dhidi ya mshtuko wa usambazaji wa kimataifa na mabadiliko ya sarafu, huku kikiboresha ushindani wa gharama za uzalishaji wa saruji”.

Kiwanda hicho kinatarajiwa kutengeneza takribani ajira 10,000 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja pindi kitakapokamilika. Zaidi ya hayo, kampuni za ndani zitafaidika kupitia fursa za kibiashara katika sekta za usafirishaji, usambazaji, uchimbaji wa mawe, na huduma za matengenezo ya vifaa.

Katika kulinda mazingira, kiwanda hicho kitatumia mfumo wa kisasa wa hatua sita (six-stage precalciner system) ili kuongeza ufanisi wa nishati na kupunguza utoaji wa hewa ukaa. Bamburi pia imepanga kutumia malighafi mbadala za kijani ikijumuisha vifuu vya nazi na taka ngumu za manispaa kutoka ukanda wa Pwani ili kuendesha majiko ya kiwanda.

Kuhusu uwajibikaji wa kijamii, Bamburi haikuwa nyuma. Imeelezwa kuwa tayari watu 112 kutoka familia 42 walioathiriwa na mradi katika Kijiji cha Mwachome wamepatiwa mafunzo ya elimu ya fedha kabla ya kupewa awamu ya pili ya fidia chini ya mradi wa kuhamishwa wenye thamani ya Shilingi milioni 250 za Kenya.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!