Latest Posts

SERIKALI YATETEA USIKILIZWAJI WA KESI YA LISSU KWA NJIA YA MTANDAO

Serikali ya Tanzania imesema kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haijakiuka sheria yoyote ilipoamua kusikiliza kesi ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, kwa njia ya mtandao.

Kauli hiyo imetolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Hamza Johari, Ijumaa hii bungeni wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

“Procedures zilifuatwa vizuri. Mtu anayesema sheria imevunjwa, aseme sheria ipi? Hii ndiyo sheria, na mimi ndiye Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” alisema Johari akijibu hoja za baadhi ya wabunge waliopinga uamuzi huo wa Mahakama.

AG Johari alifafanua kuwa kwa mujibu wa sheria, Mahakama ina mamlaka ya kufanya tathmini ya kiusalama na kuamua namna ya kuendesha kesi, ikiwemo kutumia njia ya kidigitali iwapo kuna tishio la usalama.

“Kama kuna mazingira ya hatari, kama taarifa mitandaoni zinaonyesha uwepo wa hofu au vurugu, Mahakama inaweza kuamua kesi isikilizwe kwa mtandao,” alisema.

 

Waziri wa Mambo ya Ndani: Mahakama Mtandao Itaendelea

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, naye alieleza kuwa huduma ya Mahakama Mtandao itaendelea kutumika katika mazingira yenye viashiria vya hatari, ili kulinda usalama wa watu na taasisi.

“Kama kuna maandamano yanayotishia usalama, tuna haki ya kutumia teknolojia hii,” alisema Bashungwa alipotembelea Makasha ya Mahakama Mtandao katika Gereza la Isanga, Dodoma.

 

Upinzani Wapinga Kauli ya Serikali

Kauli hizo za viongozi wa serikali zimezua mjadala mkali, hasa kutoka kwa chama cha CHADEMA. John Heche, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, alihoji kupitia mtandao wa X (zamani Twitter):

“Nilidhani uamuzi huo ni wa Mahakama, sasa Bashungwa anazungumzia kama maamuzi hayo ni ya kwao. Bashungwa ni nani kwenye kesi hii?”

Kwa upande wao, mawakili wa Lissu wakiwemo Peter Kibatala, wamepinga utaratibu wa kutumia Mahakama Mtandao, wakidai kuwa haukuwa halali kisheria na unavunja haki ya kesi kusikilizwa kwa uwazi.

 

Mzozo Mahakamani na Uamuzi Kusubiriwa

Mnamo Aprili 24, 2025, Lissu alikataa kesi yake isikilizwe kwa njia ya mtandao, akisisitiza kuwa lazima ihudhuriwe wazi. Kufuatia mabishano kati ya mawakili wa serikali na wale wa utetezi, Mahakama ya Kisutu iliahirisha kesi hiyo na kutangaza kutoa uamuzi wake Mei 6, 2025, juu ya iwapo itaendelea kwa njia ya mtandao au la.

Siku hiyo hiyo, nje ya Mahakama, kulitokea mvutano mkali kati ya Polisi na wafuasi wa CHADEMA, ambapo chama hicho kilidai kuwa takribani watu 24 walijeruhiwa na wengine, akiwemo John Mnyika na John Heche, walikamatwa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!