Latest Posts

SERIKALI YATISHIA KUTOPELEKA HUDUMA ZA KILIMO JIMBONI KWA MPINA

Serikali huenda ikasitisha kupeleka huduma za kilimo kwa wakulima wa jimbo la Kisesa, wilayani Meatu, mkoani Simiyu endapo wakulima hao wakiithibitishia serikali kuwa tuhuma zinazowasilishwa mara kadhaa na Mbunge wa jimbo hilo Luhaga Mpina (CCM) kwenye sekta ya kilimo ni sehemu ya maagizo yao.

Kauli hiyo ya serikali imetolewa na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe Septemba 11.2024 wakati akiwa kwenye siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi anayoifanya wilayani Igunga, mkoani Tabora ambapo amesema Mbunge huyo mara kadhaa amekuwa akitoa tuhuma kuwa pembejeo (dawa) za kilimo na mbegu za mazao mbalimbali zinazopelekwa na serikali kwa wakulima kuwa ni feki, sambamba na hilo amesema Mbunge huyo pia amekuwa akidai wanunuzi wanaopelekwa kununua mazao ya wakulima wanatoa bei ndogo

Kufuatia madai hayo, Waziri Bashe amesema hivi karibuni anakusudia kwenda kufanya mkutano wa hadhara na kuzungumza na wakulima wa jimbo la Kisesa ambapo atawaeleza kuwa endapo kinachozungumzwa na Mbunge Mpina ni sehemu ya maagizo yao basi serikali haitapeleka pembejeo za ruzuku, mbegu na hata wanunuzi, ili kutoa nafasi kwa Mbunge wa jimbo la Kisesa Luhaga Mpina kuwapelekea wapiga kura wake pembejeo na mbegu anazoziona kuwa bora kuliko zile zinzoletwa na serikali na kisha baada ya mavuno anunue mazao hayo hususani zao la Pamba ambalo wakulima wengi jimboni humo wanalima

“Nchi yetu tumejenga utamaduni wa watu kutuhumu bila kuleta suluhisho la matatizo, sasa hilo sio kwenye sekta ninayoisimamia mimi (sekta/wizara ya kilimo), kwa hiyo nitaenda Kisesa wakaniambie wakazi wa Kisesa kama yale mawazo ni ya kwao serikali itaondoa, lakini kama yale mawazo ni ya Mpina serikali itaendelea kuwahudumia, kwa sababu lazima tufike mahali tuweke siasa pembeni kwenye maisha ya watu, na mimi hili nimeamua kama mbaya na iwe mbaya” -Bashe

Amesema wale wote wenye dhamira ya kudhoofisha jitihada za serikali kwenye maeneo mbalimbali wasichezee sekta ya kilimo kwa kuwa kiuhalisia watu wamewekeza kodi za wananchi, muda na nguvu

Aidha, Waziri Bashe ametoa rai kwa wakulima wa Pamba nchini kuendelea kulima zao hilo kwa kuwa serikali haiwezi kuleta wanunuzi wezi (wanaowanyonya wakulima), sambamba na hilo amesema serikali haiwezi kuwaletea wakulima dawa (pembejeo) na mbegu feki

“Hatuwezi kujenga Taifa ambalo mtu anaamka tu anatukana watu asubuhi, mchana, jioni, hawa wanunuzi wa Pamba hawa mwaka 2019/2020 mnakumbuka tulivyoteseka kununua Pamba nchi hii, watu wakaenda wakafanya siasa wakasema Pamba haiwezi kuuzwa chini ya 1200 Pamba si zilidoda hapa?, si mlikopwa mnakumbuka?, si ilikuwa mateso?, wao walikuwa na shamba hata hekari moja?, sasa siruhusu huo mchezo kwenye sekta ninayoisimamia na namaanisha katika hili” -Bashe

Katika siku hiyo ya kwanza ya ziara yake ya kikazi wilayani Igunga, mkoani Tabora Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amekutana na viongozi wa Bodi ya Pamba, wafanyabiashara, wawekezaji na wakulima wa Pamba

Sambamba na hilo amezindua mpango wa kitaifa wa kuongeza tija katika uzalishaji wa Pamba katika kijiji cha Mbutu wilayani humo, sambamba na kutumia fursa hiyo kueleza mipango ya serikali ya kujenga mabwawa na miundombinu ya umwagiliaji ya kutosha na kuwahakikishia wananchi kuwa maji hayatakuwa mateso kwa wakulima wilani humo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!