Latest Posts

SERIKALI YAWASILISHA MUSWADA MPYA WA UWEKEZAJI, TIC NA EPZA KUUNGANISHWA

Katika juhudi za kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini, Serikali imewasilisha Muswada wa Sheria ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi bungeni, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa tathmini ya mashirika na taasisi za umma iliyofanyika mwaka 2023.

Akiwasilisha muswada huo siku ya Alhamisi Februari 13, 2025, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo, amesema tathmini hiyo ilionesha kuwa baadhi ya taasisi zina majukumu yanayoshabihiana, jambo lililosababisha mwingiliano wa kiutendaji na kuongeza gharama za uendeshaji wa biashara.

“Hali hii imekuwa kikwazo kwa ufanisi wa taasisi hizo na mazingira bora ya uwekezaji. Kwa kuzingatia matokeo ya tathmini, Serikali iliamua kuunganisha au kufuta baadhi ya mashirika na taasisi za umma,” amesema Prof. Mkumbo.

Miongoni mwa taasisi zilizobainika kuwa na majukumu yanayoshabihiana ni Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Kukuza Mauzo ya Bidhaa Nje ya Nchi (EPZA), ambazo sasa zitaundwa kuwa taasisi moja.

Muswada huu unalenga kuweka mfumo madhubuti wa kitaasisi kwa ajili ya uratibu, ulinzi, uvutiaji, uhamasishaji na uwezeshaji wa uwekezaji nchini, pamoja na uanzishaji, uendelezaji na usimamizi wa maeneo maalumu ya kiuchumi.

Aidha, muswada huu unapendekeza kufutwa kwa Sheria ya Uwekezaji Tanzania ya 2022, Sheria ya Maeneo Maalumu ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje ya 2002, na Sheria ya Maeneo Maalumu ya Uwekezaji ya 2006, ili kuleta mfumo mmoja unaoratibu sekta ya uwekezaji kwa ufanisi zaidi.

Serikali inatarajia kuwa mabadiliko haya yatasaidia kupunguza urasimu, kurahisisha taratibu za uwekezaji na kuvutia wawekezaji zaidi, hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!