Mbunge wa Jimbo la Lupembe mkoani Njombe Edwirn Swalle amewataka wananchi wa jimbo hilo kujivunia uwakilishi wao Bungeni kwa kuwa tangu alipoaminiwa ameweza kufanikisha upatikanaji wa miradi mingi ya maendeleo katika jimbo hilo.
Swalle ameeleza hayo wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Image kata ya Kidegembye mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa shule ya sekondari Image kwa ufadhili wa mradi wa SEQUIP ambapo amesema amesikia uwepo wa watia nia wengine ndani ya jimbo hilo na kuwataka wasijaribu kwa kuwa bado ana nguvu za kuwatumikia na wananchi walimtuma Bungeni kijana mwenye kisu kikali.
“Kwa muda mlionipa kuwatumikieni Bungeni nilihakikisha Image mnakumbukwa kwenye miradi na ndio maana mimi nilikuwa kama mtoto wenu mlienituma kwenye bucha ya Nyama na mlituma mtoto mwenye kisu kikali na ndio maana katika miaka hii minne mmefanikiwa kupata shule ya msingi,tukajenga barabara pamoja,mmefanikiwa kupata umeme,maji na tumepata shule hii mpya ya sekondari”amesema Swalle
Ujenzi wa shule hiyo mpya iliyosajiliwa kwa mkondo wa amali utasaidia kupunguza changamoto ya wanafunzi wa Image kufuata elimu umbali mrefu pamoja na kupata maarifa,stadi na ujuzi ambapo mpaka sasa kiasi cha zaidi ya Milioni 581 kimekwishatumika katika ujenzi wa shule hiyo.