Wamiliki wa maeneo mbalimbali mkoani Mtwara wametakiwa kuhakikisha wanazuia ujenzi unaofanywa na wananchi wasiokuwa wamiliki halali wa maeneo hayo ili kuepuka migogoro.
Akizungumza kwenye kikao kilichowakutanisha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa na wilaya za Mtwara pamoja na makamishna wasaidizi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo, amesema migogoro mingi hutokea kutokana na ukosefu wa usimamizi wa taasisi mbalimbali zinazomiliki maeneo hayo.
Amesema taasisi zote nchini zinapaswa kusimamia ipasavyo maeneo yao na kuzuia uvamizi ili kuepuka migogoro ya baadaye, jambo ambalo litasaidia wizara kushughulikia tu matatizo ambayo tayari yapo.
“Nitoe wito kwa taasisi zote nchini kulinda maeneo yao. Tusipofanya hivyo, migogoro ikizidi kuongezeka itakuwa tatizo kubwa kwa wizara. Wakitusaidia katika hilo, sisi tutajipanga kukabiliana na ile iliyo tayari ipo.” Amesema Akwilapo
Aidha, Waziri Akwilapo amepongeza uongozi wa mkoa na wilaya kwa kufanya majadiliano, akisema hatua hiyo inazingatia kazi na utu kwa kuwa wananchi wamekuwa wakitumia maeneo hayo kwa muda mrefu.
Hata hivyo, amesema kutokana na uwepo wa migogoro saba, wizara italeta timu itakayoongozwa na Kamishna ambayo itafanya uchunguzi na kuwasilisha ripoti itakayoonesha mapendekezo ya wizara.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Bahati Geuzye amesema wamefarijika na kauli ya Waziri ya kuimarisha juhudi za kumaliza migogoro hiyo, na amemhakikishia kuwa wako tayari kutekeleza maagizo yote aliyotoa, hususan ya kulinda maeneo yao ili kuzuia kutokea kwa migogoro mipya.