Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Tabora imefanikiwa kukamata mabelo ya magunia 2,681 ya kufungia Tumbaku yaliyotumika (MAJAFAFA) yenye thamani ya shilingi bilioni 1.4 kutoka kwa wafanyabiashara waliokuwa wakiyauza kinyume na utaratibu kwa kipindi cha Januari – Machi 2025.
Taarifa hiyo imetolewa na Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Tabora, Azza Mtaita wakati akizungumza na waandishi wa habari tarehe 27 Mei 2025, amesema kwa kushirikiana na vyombo vya dola watuhumiwa saba wa sakata hilo walifikishwa mahakamani ambapo baadhi yao wamekubali kufanya makubaliano ya kulipa fedha kufidia hasara waliyoisababishia serikali na kurudisha magunia kwa wakulima.
Jumla ya magunia 1,315 tayari yamerejeshwa kwa wakulima kati ya 2,681 yaliyokamatwa kupitia vyama vyao vya msingi vya Mulokhu, Mkombozi, Bukemba, Ikobelo na Kasisi, na kwamba taratibu zingine zinaendelea kuhakikisha magunia yote yanarudishwa kwa wakulima.
Katika hatua nyingine, TAKUKURU Mkoa wa Tabora imefuatilia utekelezaji wa miradi 14 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi 45,953,955,952.57, kati ya miradi hiyo, miradi 4 yenye thamani ya shilingi 17,805,893,608.15 ambayo ilikuwa na mapungufu mbalimbali ambayo maelekezo yametolewa kufanyiwa kwa marekebisho.
Sambamba na hayo, jumla ya malalamiko 116 yalipokelewa ambapo 92 yalihusu rushwa, taarifa 4 zilihamishwa, 20 walipewa ushauri, taarifa 12 uchunguzi wake unaendelea, huku mashitaka ya kesi 4 yakifungiliwa, kesi 3 ziliamriwa ambapo Jamhuri ilishinda kesi 1, ilishindwa kesi 1 na kesi 1 iliondolewa, na kesi 15 bado zinasikilizwa katika mahakama za mkoa wa Tabora.
Hata hivyo, Azza amesema kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu wataendelea kushirikiana na wadau wa uchaguzi ili kuhakikisha wanazuia kutokea kwa vitendo vya rushwa kabla, wakati na baada ya uchaguzi.