Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ) kimeonya kuhusu hali ya kukithiri kwa vitendo vya udhalilishaji dhidi ya watoto na kuomba hatua kali za kisheria kuchukuliwa dhidi ya wahalifu.
TAMWA ZNZ imeeleza kuwa ripoti ya hivi karibuni kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar inaonesha matukio 165 ya ukatili wa kijinsia yaliyoripotiwa mwezi Julai 2024, ambapo watoto walikuwa waathirika wakuu.
Katika ripoti hiyo, watoto walihesabuwa kuwa 142, sawa na asilimia 86.1 ya waathirika wote, huku wasichana wakiwa 115 (asilimia 81.0) na wavulana 27 (asilimia 19.0). TAMWA ZNZ imesema hali hii inahitaji udhibiti mkali kutoka kwa wadau wote, ikiwa ni pamoja na Serikali, taasisi za kijamii, wazee, walimu, na watoto wenyewe.
“Tunaona hali hii ni ya kusikitisha na inahitaji kudhibitiwa kwa nguvu zote. Wasimamizi wa watoto wanapaswa kuhakikisha haki za watoto zinazingatiwa na adhabu kali zichukuliwe dhidi ya wahalifu wa vitendo vya ukatili kwa mujibu wa sheria.” Wameeleza TAMWA ZNZ.
TAMWA ZNZ pia imetolea mfano tukio la hivi karibuni ambapo mtoto wa miaka miwili alikamatwa pamoja na mlezi wake na watendaji wa Manispaa ya Magharibi ‘A’ kwa kisingizio cha wazazi wake kutolipa ada ya usafi.
“Kitendo hiki kilizua taharuki kwa familia ya mtoto na jamii kwa ujumla, na kimeenda kinyume na haki za mtoto pamoja na haki za binaadamu,” wamesema TAMWA ZNZ.
Sheria ya Mtoto ya Zanzibar Na 6 ya mwaka 2011 inapinga udhalilishaji wa watoto wa aina yoyote ili kukuza ustawi wao. Aidha, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watoto (UNCRC) wa mwaka 1989, ambao Tanzania na Zanzibar wameuridhia, unasisitiza kulinda haki za watoto.
“Tunatoa wito kwa jamii kuwalinda watoto wetu na kuhakikisha hawakumbwi na vitendo vya udhalilishaji. Ni jukumu letu sote kulinda haki za watoto na kuhakikisha wanakua katika mazingira salama,” wamesema TAMWA ZNZ.