Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila MKumbo pamoja na ujumbe anaouongoza katika safari ya kutembelea viwanda na miradi mbalimbali ya Dangote, jijjni Lagos, Nigeria, leo amekutana na uongozi wa Dangote Group na kujadiliana masuala mbalimbali ya biashara na uwekezaji nchini Tanzania.
Katika kikao hicho mambo yaliyojadiliwa ni fursa zilizopo nchini katika masuala ya biashara na uwekezaji yakiwemo, mradi wa Bandari ya Bagamoyo na Kongani ya viwanda, uzalishaji wa mbolea, pamoja na kuvua umeme kwa kutumia makaa ya mawe.
Akizungumza katika Mkutano huo Makamu wa Rais wa Dangote Group, DVG Edwin alitaka kufahamu mifumo na haki zilizopo kwa wawekezaji hususani kwenye ardhi, madini na masuala ya uzalishaji umeme, ambapo Prof. Kitila alimuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka za Uwekezaji na Maeneo Maalumu Tanzania (TISEZA) pamoja na Wakuu wa Taasisi walioshiriki ziara hiyo chini ya sekta husika na timu ya kiufundi kukutana na uongozi wa Dangote na kutoa ufafanuzi wa kina kwenye masuala hayo.
