Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umeendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa wananchi wa Mkoa wa Iringa kupitia uboreshaji wa miundombinu ya barabara, kwa kutumia bajeti ya Shilingi Bilioni 68 iliyotengwa kwa kipindi cha mwaka 2021 hadi 2025.
Akizungumza wakati wa kikao cha uwasilishaji wa utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa halmshauri Kuu ya CCM Mkoa wa Iringa kwa mwaka 2020-2025 ,Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Peter Serukamba, alisema kuwa barabara nyingi za lami zilizojengwa kupitia bajeti hiyo zimeleta manufaa makubwa kwa wakulima na wafanyabiashara wa mkoa huo.
“Barabara hizi zimekuwa mkombozi mkubwa kwa wakulima wa chai, nyanya, mboga mboga na mazao mengine ya kilimo. Sasa mazao yanafikishwa sokoni kwa haraka bila kuharibika mashambani, jambo ambalo limepunguza hasara na kuongeza kipato cha wananchi,” alisema Serukamba.
Aliongeza kuwa mafanikio ya TARURA yamechangia kupunguza gharama za usafirishaji, kuongeza tija kwa wakulima na kuchochea ukuaji wa uchumi katika maeneo ya vijijini.
Wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM Mkoa wa Iringa waliunga mkono taarifa hiyo na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza kwenye barabara nyingine zenye mchango wa kiuchumi.
Pia walitoa wito kwa serikali kuharakisha ujenzi wa barabara ya Mafinga–Mgololo, wakibainisha kuwa Wilaya ya Mufindi inaongoza kwa uzalishaji wa miti na mazao ya misitu, ambayo bado yanakumbwa na changamoto za usafirishaji kutokana na miundombinu duni.
Nao wananchi wameeleza kuridhishwa kwao na juhudi hizo, wakisema zimewapa matumaini mapya ya kiuchumi.
“Tunaweza kuuza nyanya zetu bila hofu ya kuoza njiani. Barabara nzuri ni suluhisho kubwa kwa sisi wakulima,” alisema Elibeth Kavenuke, mkulima kutoka Wilaya ya Iringa.
Utekelezaji wa miradi ya TARURA umeendelea kuwa mfano hai wa utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa vitendo, huku mabadiliko katika maisha ya kila siku ya wananchi yakionekana wazi.