Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), kwa kushirikiana na Kituo cha Msaada wa Kisheria Ngorongoro (NGOLAC), wamekabidhi msaada wa magodoro na vifaa vingine katika gereza la Loliondo kwa ajili ya wafungwa na mahabusu.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Mratibu Kitaifa wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa, amesema msaada huo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha haki za binadamu kupitia misingi ya haki jinai. Amehimiza mashirika na wadau wengine kuunga mkono jitihada hizi kwa kutoa huduma kwa wafungwa na mahabusu kama sehemu ya kuimarisha haki jinai nchini.
Wakili Olengurumwa pia amepongeza uongozi wa gereza la Loliondo kwa kuweka mazingira safi na mazuri ambayo yanawasaidia wafungwa kupata mafunzo muhimu kama vile kutunza bustani, ufundi seremala, na ujenzi. Aliongeza kuwa mafunzo haya yanachangia katika kuwaandaa vizuri wafungwa kwa maisha ya baada ya kifungo.
Aidha, Wakili Olengurumwa ametembelea tarafa ya Ngorongoro kufuatilia utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kurudisha huduma za kijamii. Amezungumza na wananchi, viongozi wa Halmashauri na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kuhusu masuala ya huduma kwa jamii na umuhimu wa kufanyika kwa uchaguzi katika vijiji vilivyofutiwa zoezi hilo.
Mkuu wa Gereza la Loliondo, SP George Osindi, pamoja na uongozi wa gereza, wameishukuru THRDC na NGOLAC kwa msaada wao, wakibainisha kuwa vifaa hivyo vimekuja wakati wa uhitaji mkubwa. Ameongeza kuwa msaada kama huu unasaidia kuboresha mazingira ya wafungwa na mahabusu na kutoa wito kwa mashirika mengine kufuata mfano huo wa kusaidia.
THRDC ipo kwenye ziara ya kutembelea wanachama wake wa kanda ya kaskazini, mikoa ya Manyara, Arusha, na Kilimanjaro. Ziara hiyo inalenga kuona ofisi za wanachama, kushuhudia kazi zao, kujadili changamoto zinazowakabili na kuwakumbusha majukumu yao kama wanachama wa mtandao huo.