Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kinashiriki katika Mkutano wa Dunia wa Mabadiliko ya Tabianchi unaofanyika jijini Baku, Azerbaijan kuanzia Novemba 11 hadi 22, 2024. Lengo la ushiriki huo ni kuhamasisha wawekezaji na sekta binafsi kuwekeza nchini Tanzania katika miradi inayolenga kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Katika mkutano huo, Tanzania imejipambanua kwa kuwa na eneo maalum la kujinadi lijulikanalo kama Tanzania House, ambapo Kituo cha Uwekezaji (TIC) kilipata fursa ya kumpa taarifa Dkt. Phillip Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alipotembelea eneo hilo kuhusu mipango ya kuitangaza nchi na kunadi miradi ya kijani inayolenga kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
TIC imefanya mazungumzo na kampuni mbalimbali zinazojihusisha na uwekezaji katika sekta zinazolenga kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ikijumuisha uzalishaji wa nishati mbadala kwa teknolojia rafiki kwa mazingira, kilimo endelevu kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi, miradi ya kaboni krediti kwa uhifadhi wa mazingira, viwanda visivyo na athari kubwa kwa mazingira na huduma za kifedha zinazosaidia miradi ya kijani.
Hatua hizi zinajibu jitihada za Tanzania zilizoainishwa katika Sera ya Taifa ya Mazingira na Mkakati wa Mabadiliko ya Tabianchi, unaolenga kuiwezesha nchi kuhimili na kushiriki katika jitihada za kimataifa za kupambana na mabadiliko ya tabianchi huku ikifikia maendeleo endelevu.
Kwa mujibu wa TIC, lengo ni kuhakikisha kwamba angalau asilimia 10 ya miradi yote inayosajiliwa ni inayohusu kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Hatua hii inalenga kuchangia katika juhudi za kitaifa za kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kuchochea maendeleo endelevu.