Rais wa Marekani, Donald Trump, na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, wamefanya mkutano na waandishi wa habari ambapo Trump ametoa pendekezo la Marekani kuichukua Gaza chini ya udhibiti wake na kuwahamisha watu milioni 1.8 wa Gaza kwenda nchi nyingine za Kiarabu.
Trump amesema kwamba baada ya Marekani kuijenga upya Gaza, inaweza kuwa makazi ya “watu wa dunia nzima”.
Alipoulizwa na wanahabari ni kwa mamlaka gani Marekani inaweza kudhibiti Gaza, Trump hakutoa majibu ya moja kwa moja, lakini alieleza kuwa anaona “hati miliki ya muda mrefu” juu ya eneo hilo.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alikubaliana na wazo la Trump na kumuita “rafiki mkubwa wa Israel”.
Katika mkutano huo, Trump pia alimkosoa mtangulizi wake Joe Biden, akidai kuwa Biden alimfanya Israel kuwa dhaifu kwa kuruhusu maadui wake kuwa na nguvu zaidi katika kipindi chake cha miaka minne madarakani.
Msemaji wa Hamas amekosoa pendekezo hilo, akilitaja kuwa “mpango wa kuleta machafuko”, akisisitiza kuwa Wapalestina wa Gaza hawatakubali kuondolewa kwao. Kulingana na Hamas, suluhisho la kweli ni kumaliza vita na kuachana na mipango ya kuwahamisha raia wa Gaza.
Netanyahu ni kiongozi wa kwanza wa kigeni kutembelea Washington wakati wa muhula wa pili wa Trump katika Ikulu ya White House.