Latest Posts

UBELGIJI YAUNGA MKONO KAMPENI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA, YAJIPANGA KUSHIRIKIANA NA TANZANIA

Ubelgiji imesema inaunga mkono Kampeni ya Nishati Safi ya Kupikia iliyoanzishwa na Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na ina nia ya kushirikiana na Tanzania katika kukuza matumizi ya nishati hiyo kwa maendeleo ya Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla.
 
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nishati wa Ubelgiji, Tinne Van der Straeten katika kikao na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati wa Tanzania, Dkt. Doto Biteko kilichofanyika mjini Windhoek, Namibia, kama sehemu ya Mkutano wa Nchi za Afrika unaojadili matumizi ya Hydrojeni kuzalisha umeme.
 
Waziri Tinne amesema kuwa nchi ya Ubelgiji iko tayari kuunga mkono jitihada za matumizi ya nishati safi ya kupikia, kwani ni mkakati wa kimataifa wa uhifadhi wa mazingira na kuwawezesha wananchi kukuza pato na maendeleo ya kiuchumi.
 
Kwa upande wake Dkt. Biteko amesema ili kupata maendeleo ya kweli, Tanzania inatoa kipaumbele katika matumizi ya nishati ambayo itawawezesha kupata maendeleo endelevu ikiwa ni pamoja kuondokana na magojwa na vifo vinavyotokana na matumizi ya nishati isiyokuwa safi.
 
Amesema ushirikiano wa miaka mingi kati ya Tanzania na Ubelgiji utawezesha upatikanaji wa maendeleo yanayoweza kutokana na uwekezaji wa kimkakati kutoka kwa wafanyabiashara na wawekezaji.
 
“Tanzania kupitia Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeasisi na inaendeleza kampeni kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia katika kipindi cha miaka 10 ijayo.” Ameeleza Dkt. Biteko.
 
Mkutano wa Hydrojeni nchini Namibia unalenga kuibua fursa na changamoto za matumizi ya nishati hiyo, ambapo Tanzania inapata fursa ya kujifunza matumizi ya Hydrojeni katika uzalishaji wa umeme. Mkutano huo unatarajiwa kuhitimishwa tarehe 5 Septemba 2024.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!