Ujenzi wa jengo la abiria katika uwanja wa ndege wa Arusha umefikia asilimia 98 huku ujenzi wake ukiambatana na usimikaji wa mifumo ya usalama, kuongozea ndege pamoja na usalama.
Mbali na kukamilika kwa jengo hilo, Serikali ina mpango wa kuendelea na maboresho mbalimbali katika uwanja huo ikiwemo uwekaji wa taa za kuongezea ndege ili kuuwezesha uwanja huo kutumika usiku na mchana.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile alipotembelea kujionea mwenendo wa kazi za ujenzi wa jengo hilo.
Naibu Waziri Kihenzile ameongeza kwa kusema kuwa, maboresho yanayofanywa katika uwanja wa ndege wa Arusha pamoja na malengo mengine, yanalenga kukuza sekta ya utalii, sekta ambayo inategemewa na serikali katika kuingiza fedha nyingi za kigeni.
“Uwanja wa ndege wa Arusha ni moja ya viwanja vikubwa na muhimu kwa taifa letu, na pia kama tunavyofahamu kuwa, nchi yetu inategeme sekta ya utalii katika kuingiza fedha nyingi za kigeni, na ukizungumza utalii unazungumzia Kaskazini, na ukizungumzia Kaskazini unazungumzia Arusha, hivyo uwanja huu ni muhimu na wa kimkakati” alisema Naibu Waziri Kihenzile
Vilevile amesema, ujenzi wa jengo hilo la abiria unatarajiwa kukamilika na kuanza kutumika mwezi huu wa Septemba.
“Ninayo furaha kuwatangazia na kuwaambia wananchi kuwa, jengo hili la abiria ambalo limejengwa na serikali hii ya awamu ya sita kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 8.2 lipo asilimia 98 na tunategemea mwezi huu wa Septemba, 2024 litaanza kutumika ili wananchi waendelee kunufaika na uwekezaji huu” Aliongeza Naibu Waziri huyo.
Kufuatia hilo, ameipongeza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kwa usimamizi mzuri na ujenzi wa jengo hilo, na kujibu swali ambalo lilikuwa linauzwa bungeni na wabunge wa Mkoa wa Arusha, mikoa ya jirani pamoja na mikoa mingine hapa nchini, wakihoji ujenzi huo utakamilika lini?
Uwanja wa ndege wa Arusha ni uwanja wa pili kwa miruko mingi ukitanguliwa na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Aidha, uwanja wa ndege wa Arusha unaingizia Serikali fedha nyingi kutokana na upokeaji wake wa idadi kubwa ya watalii.