Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) limetangaza kuwa maelfu ya wafanyakazi wake wataondolewa kazini kwa muda kuanzia Ijumaa usiku, hatua inayotokana na sera mpya za utawala wa Rais Donald Trump.
Katika taarifa rasmi iliyotolewa na shirika hilo, wafanyakazi wa moja kwa moja wa USAID ndio watakaoathirika, isipokuwa wale waliopo kwenye nafasi za uongozi, kazi muhimu, na programu maalum. Hata hivyo, haijabainika ni kazi zipi hasa zitakazoathirika.
USAID imesema kuwa wafanyakazi wote watajulishwa kufikia Alhamisi mchana kuhusu hatma yao. Serikali ya Trump imeeleza kuwa USAID inafuja pesa za walipa kodi na inahitaji kufanyiwa mabadiliko ili kuendana na vipaumbele vya sera za rais.
Hatua hiyo imeibua malalamiko kutoka kwa wafanyakazi wa shirika hilo, ambao wakiungwa mkono na wabunge wa chama cha Democratic, wameandamana kupinga uamuzi huo. Wanasema kuwa kuondolewa kazini kwa maelfu ya wafanyakazi kutahatarisha maisha ya watu wanaotegemea misaada ya USAID na pia kuhatarisha usalama wa taifa.
Kwa mujibu wa tovuti ya USAID, shirika hilo litashirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kuhakikisha wafanyakazi waliotumwa nje ya nchi wanarejea ndani ya siku 30, kwa gharama ya serikali.
USAID, ambalo ni moja ya mashirika makubwa ya misaada ya kimataifa, linaajiri takriban watu 10,000 duniani kote, huku theluthi mbili wakihudumu nje ya Marekani.
Shirika hilo lililoanzishwa mwaka 1961, lina bajeti ya takriban dola bilioni 40 kwa mwaka, kiasi kinachokadiriwa kuwa 0.6% ya bajeti ya serikali ya Marekani.