Baadhi ya wakazi wa tarafa za Loliondo na Sale wilayani Ngorongoro mkoani Arusha wanadaiwa kushikiliwa na Jeshi la Polisi Wilayani humo kwa kile kinachoelezwa kuwa hatua inayotokana na wao kutoka hadharani kuomba kuundwa kwa tume jumuishi ya kutatua migogoro katika wilaya yote ya Ngorongoro na si katika baadhi ya tarafa.
Wananchi hao ni sehemu ya wanawake waliotoa maoni yao kutokana na tume mbili zilizoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan mwanzoni mwa mwezi huu kwa lengo la kushughulikia changamoto za wananchi wa wilaya ya Ngorongoro.
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umedai kuwa mbali na wananchi hao kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kipindi cha muda fulani, wengine wameandikiwa barua ya kuitwa katika kikao cha kamati ya usalama wilaya.
“Kinachotushangaza ni kwamba wananchi wa Loliondo ambao wametoa maoni yao kama Watanzania wengine wameitwa polisi, Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Wilaya ya Ngorongoro ameitwa polisi kwa kutoa maoni yake, akawekwa ndani kwa muda mchache” ameeleza Wakili Onesmo Olengurumwa, Mratibu wa Kitaifa wa THRDC.
THRDC imeeleza kusikitishwa na kulaani vitendo hivyo vinavyodaiwa kufanyika wilayani Ngorongoro ikivitaja kuwa “vitisho dhidi ya wananchi na watetezi ambao wamekuwa wakiisemea jamii”.
Katika tamko walilolitoa hivi karibuni, wananchi hao wamesema kuwa katika tume zote mbili zilizoundwa na Rais Samia hazijagusa wilaya nzima ya Ngorongoro hasa tarafa za Loliondo na Sale, badala yake imeegemea upande mmoja wa tarafa ya Ngorongoro, hali waliyoieleza kutokuwa sawa kwani hata tarafa za Loliondo na Sale kuna changamoto ya migogoro ya ardhi na uwekezaji, hivyo kumuomba Rais kuunda tume nyingine itakayoshughulikia changamoto za tarafa hizo.
Aidha wananchi hao pia walimuomba Rais Samia kuwa wanataka kuona wawakilishi wa wananchi kutoka tarafa zote tatu wakishiriki kwa asilimia kubwa kuunda tume hizo pamoja na Asasi Za Kiraia, viongozi wa mila na viongozi wa kidini badala ya tume hizo kuundwa kwa wingi na watu waliopo kwenye mfumo wa serikali.
THRDC imeeleza kuwa wananchi hao walitumia haki yao ya kikatiba ya kutoa maoni kama ambavyo wananchi wengine, wachambuzi wa masuala ya siasa na uraia, na taasisi zingine zilivyofanya katika majukwaa mbalimbali ikiwamo runinga na mitandao ya kijamii mara baada ya Rais Samia kuunda tume hizo.
“Tume hizi zinakwenda kugusa maisha yao kama wananchi wa wilaya ya Ngorongoro, hivyo ilikuwa ni haki kwa wananchi wa Ngorongoro kwanza kupongeza uwepo wa tume hizi kama walivyofanya, lakini kwenda mbali zaidi kutoa maoni kuhusu nuundo wa tume hizi”, ameeleza Wakili Olengurumwa.
Olengurumwa amewaomba viongozi wa Loliondo na Ngorongoro kwa ujumla kuepuka kuwaingiza wananchi wao katika mtanzuko na mazingira ambayo watahisi wanaendelea kuonewa akieleza kuwa hawakufanya kosa lolote kutoa maoni yao ambayo waliyaelekeza kwa Rais Samia.
Hata hivyo, Jambo TV tumemtafuta Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ngorongoro Leah Ncheyeki ambaye yeye ameeleza kutokuwa na taarifa ya kukamatwa kwa wananchi hao hali iliyotulazimu kumtafuta Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya.
Tumempigia simu DC wa Ngorongoro, Kanali Wilson Sakulo ambaye hakupokea simu lakini akatujulisha kwa maandishi baada ya kumtumia ujumbe kwa njia ya simu, ambapo amesema “hakuna aliyekamatwa”.