Latest Posts

WAFANYAKAZI KIWANDA CHA CHAI NJOMBE WAGOMEA KAZI KISA KUTOLIPWA KWA MIEZI MINNE

News, Njombe.

Wafanyakazi wa kiwanda cha chai cha Kampuni ya DL Group kilichopo mtaa wa Kibena kata ya Ramadhani mkoani Njombe ikiwamo wachumaji wa majani ya chai wamesimamisha ufanyaji kazi na kupelekea shughuli zote za uzalishaji kusimama wakishinikiza kulipwa stahiki zao ikiwamo mshahara wa miezi minne.

Jambo TV imefika kiwandani hapo na kukuta wafanyakazi wakiwa wamekusanyika nje ya geti la kiwanda ambapo wamedai kuwa kutolipwa mshahara wao miezi minne (4) kumesababisha maisha yao kuwa magumu kwa kushindwa kumudu mahitaji muhimu ya familia ikiwamo kutowapeleka watoto shuleni huku pia mtaani wakishindwa kukopesheka.

“Tunataka mishahara yote ya miezi minne na NSSF yetu ya miaka mitano, tumetumika na kudanganywa vya kutosha na tumevumilia lakini sasa uvumilivu umeishia hapa, yaani tumezua picha mbaya hadi shuleni ‘wafanyakazi wa kibena ni wasumbufu kutoa michango’ na tukienda mtaani kukopa wanasema ‘wewe mfanyakazi wa chai hatukukopeshi” Amesema Chesco Mligo.

Aidha licha ya jitihada zilizofanyika za kukutana na meneja wa kiwanda hicho, Gerad Ngenzi amesema hawezi kuzungumza lolote kwani msemaji wa kampuni hayupo katika eneo hilo.

Hata hivyo siku kadhaa zilizopita Mkurugenzi wa Kampuni ya DL Group, David Lingat akizungumza wakati wa kikao na Mkuu wa Mkoa wa Njombe Anthony Mtaka alisema kuna changamoto ya biashara ya chai si katika kampuni hiyo pekee bali katika sekta ya chai lakini wanaweka mikakati ya kutafuta suluhisho kwa kushirikiana na serikali ili waweze kutatua changamoto.

 

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!