Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu JK Nyerere mkoani Mara, inatarajia kuanza kutoa huduma ya mgongo wazi pamoja na vichwa vikubwa kwa watoto baada ya kukamilika kwa mafunzo yatakayotolewa na madaktari bingwa kutoka hospitali ya kanda ya Bugando.
Daktari Bingwa wa upasuaji wa ubongo na mgongo kutoka hospitali ya kanda ya Bugando Dkt. Gerald Mayaya amesema wameanza kutoa huduma hiyo inayoendana na mafunzo ili kusaidia wananchi kupata huduma karibu.
“Lengo kubwa ni kusaidia madaktari waweze kutoa huduma kwa watoto wanaokuja, mfano kama Bugando tunaona watoto 700 kwa mwaka lakini kati ya hao watoto 50 wanatokea mkoa wa Mara, kwa hiyo wakiwa na uwezo wa kuwahudumia itasaidia kupunguza rasilimali muda na fedha”, amesema Dkt. Mayaya.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mwanangu Development Tanzania, Walter Miya amesema lengo la kutoa mafunzo hayo kwa hospitali za rufaa za mikoa ni kuhakikisha wanawajengea uwezo madaktari wakutoa huduma kwa wananchi wa mkoa wa Mara na maeneo mengine huku baadhi ya wananchi walionufaika na huduma hiyo wakipongeza kwani imesaidia kuboresha na kutoa unafuu wa maisha kwa watoto wao.