Zaidi ya walimu 3,900 wa elimu ya mafunzo ya ufundi na ufundi stadi nchini wameanza kupatiwa mafunzo ya Mfumo Mpya wa Umahiri yanayotolewa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa njia ya masafa kupitia Programu ya Elimu na Ujuzi kwa Ajira (ESPJ II).

Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea walimu uwezo na mbinu za kisasa za ufundishaji na ujifunzaji, ili waweze kutoa mafunzo yenye ubora na yanayokidhi mahitaji ya soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Akizungumza kuhusu mafunzo hayo, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC), Dkt. Andrew Damian Boi, amesema mafunzo hayo yamewalenga walimu wa ufundi na ufundi stadi kutoka vyuo vya ufundi stadi, vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC) pamoja na shule za sekondari zinazotoa masomo ya mkondo wa amali.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mafunzo ya Muda Mrefu na Muda Mfupi kwa Watumishi wa VETA, Judith Kimaro, amesema awamu ya kwanza ya mafunzo hayo inaendeshwa kwa njia ya mtandao, huku awamu ya pili ikitarajiwa kufanyika ana kwa ana.
Nao baadhi ya wakufunzi walioshiriki mafunzo hayo wameeleza kuwa mfumo huo mpya wa umahiri utakuwa na tija katika kuboresha ufundishaji na ujifunzaji, kuongeza ufanisi kwa walimu pamoja na kuhakikisha wahitimu wanapata ujuzi unaoendana na mahitaji halisi ya soko la ajira.
