Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Nkomi, amewataka wananchi kushiriki kikamilifu kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma Kitaifa yatakayofanyika kuanzia tarehe 16 hadi 23 Juni 2025 katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Nkomi amebainisha hayo Jumatano Mei 28,2025 Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea katika Maadhimisho hayo yenye kauli mbiu isemayo “Himiza Matumizi ya Mifumo ya Kidijiti ili Kuongeza Upatikanaji wa Taarifa na Kuchagiza Uwajibikaji”
Aidha amesema huduma mbalimbali muhimu zitapatikana moja kwa moja kupitia taasisi za umma ni pamoja na usajili wa vyeti vya kuzaliwa, utoaji wa vitambulisho vya taifa (NIDA), hati za viwanja, pamoja na huduma za afya kutoka hospitali ya Benjamin Mkapa, JKCI, Muhimbili na MOI. Pia kutakuwepo na huduma ya Gazeti la Serikali na maonesho ya huduma za taasisi mbalimbali.
“Tunaalika wananchi wote, hususani wa Dodoma na maeneo ya jirani, pamoja na watumishi wa umma kujitokeza. Hii ni fursa muhimu ya kupata huduma kwa karibu, kujifunza na kuelewa matumizi ya mifumo ya kidijitali katika kuboresha huduma za umma,” amesema Nkomi.
Amesema lengo la maadhimisho haya ni kutambua mchango wa watumishi wa umma katika maendeleo ya taifa, kuhimiza ubunifu, kupokea mrejesho kutoka kwa wananchi na kuandaa utumishi kuhimili changamoto za siku zijazo.
” Wananchi wataweza pia kufahamu haki na wajibu wao, huku taasisi za umma zikipata fursa ya kubadilishana uzoefu, kuonyesha mafanikio na kuboresha utoaji wa huduma kwa manufaa ya wote,” Amesema .
Hata hivyo , amewakumbusha watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kushiriki katika zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, akisisitiza kuwa ni wajibu wa kikatiba kuhakikisha kila Mtanzania anashiriki kikamilifu katika kuchagua viongozi bora.
“Hii ni hatua muhimu ya kuhakikisha kila raia anatimiza haki yake ya msingi ya kupiga kura na kushiriki katika mchakato wa kidemokrasia,” ameongeza.