Na Theophilida Felician, Kagera.
Umoja wa wanandembo nchini umeelezea juhudi zinazofanyika kufanya maombi wakiiombea nchi ili kufanikiwa salama zoezi muhimu la uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu 2025.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa umoja huo taifa Omulangi Domina Angribelt Abraham akiwa na baadhi ya wanaumoja baada ya kuweka kibao chenye utambulisho wa huduma zao katika mzunguko wa barabara kuu ya Uganda road kata Rwamishenye manispaa ya Bukoba.

Mwenyekiti Domina amesema kuwa wao ni watu wanaotoa huduma ya maombezi kwa jamii kupitia ibada za asili kwa sasa wamejikita kuliombea amani na utulivu taifa kama ilivyo kwa watu wengine hususani viongozi wa dini na taasisi mbalimbali zenye kuihamasisha amani.
Amefafanua kwamba amani ni msingi wa taifa lolote duniani hivyo watanzania hawanabudi kuungana pamoja na kuilinda kwa uchungu na nguvu zote.
Majukumu ya wanandembo Domina ameyataja kuwa ni pamoja na kuhamasha jamii kuenzi na kuhifadhi mila na desturi, kufundisha upendo, maadili yanayohusu familia, jamii na taifa pamoja na kuweka msukumo kwenye mafunzo ya kijamii yenye asili ya kitamaduni ambapo wamefanikiwa kuwafikia wananchi wengi wanaojitokeza maeneo yao maalumu (Murulembo) kata Kashai kupata tiba ya maombezi wakiwemo wagonjwa na wenye changamoto kadha wa kadha

Hata hivyo ameongeza kwamba wanafanya hivyo kumuunga mkono Chifu mkuu Hangaya ambaye ni Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutokana nania yake njema ya kuunga mkono suala la mila na desturi ambazo zimeanza kupotea kwenye jamii zetu.
Ameishukuru serikali ngazi ya taifa, mkoa na wilaya kwa namna inavyoshirikiana nao ili kuhakikisha shughuli zao zinaendelea vizuri bila ya vikwazo.
Mwenyekiti huyo akiambatana na mwenyekiti wa umoja huo kwa mkoa kagera Donatha Pangarace, baadhi ya waamini wake na balozi wa umoja, pamoja wamesisitiza suala la kuzingatia maadili wakifafanua kwamba kwa sasa kiwango cha maadili kimepungua kwenye jamii makundi yote watoto kwa wakubwa hali siyo nzuri.
Balozi wa wanandembo Richard Leonard Mushashu amebainisha kuwa kushuka kwa maadili kumechangia baadhi ya matukio maovu ya wizi, ulevi, mauaji na mifarakano katika familia ambapo amesisitiza jamii iludi kwenye mstari na kuzingatia mila na desturi zinazosaidia kuijenga jamii iliyo bora.