Latest Posts

WANUFAIKA WA MIKOPO YA 10% SERENGETI WAAHIDI KUZITUMIA FEDHA KWA TIJA

Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti imekabidhi jumla ya shilingi milioni 360 kwa vikundi 53 vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu kupitia mpango wa mikopo ya asilimia 10.

Hafla ya kukabidhi hundi kwa wanufaika hao imefanyika Desemba 06, 2024, ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Kemirembe Lwota ambapo akizungumza wakati wa hafla hiyo, amewataka wanufaika wa mikopo hiyo kuhakikisha wanaitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ya kukuza uchumi wao badala ya kutumia fedha hizo kwa starehe.

“Msitumie fedha hizi kwa matumizi ya binafsi. Zitumikeni kulingana na maandiko ya miradi yenu. Onesheni kwa vitendo kuwa mikopo hii ina manufaa kwa kuboresha maisha yenu kupitia biashara,” amesema Lwota.

Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuinua hali ya kiuchumi ya wananchi wake kupitia mikopo isiyo na riba, na akasisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili ya matumizi ya fedha hizo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Mujibu Babara, amewakumbusha wanufaika kuhusu viapo walivyoapa wakati wa kuchukua mikopo hiyo. Amewataka kuhakikisha wanarejesha mikopo hiyo kwa wakati ili wengine nao wanufaike.

“Bila nyie kurejesha, hakuna namna wengine wataweza kukopeshwa. Nidhamu ya fedha ni muhimu,” amesema Babara.

Baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo wameishukuru Serikali kwa kuwarudishia mpango huu wa mikopo na wakaahidi kuzitumia fedha hizo kwa tija katika biashara zao ili waweze kurejesha mikopo hiyo kwa wakati.

Kwa awamu hii ya kwanza, kiasi cha shilingi milioni 360 kimetolewa kwa vikundi 53, huku mpango huo ukiwa ni sehemu ya jitihada za Halmashauri hiyo katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia mikopo isiyo na riba.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!