Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, ameishutumu CHADEMA kwa kile alichodai kuwa chama hicho kimekuwa kikiwatumia vijana wa Tarime kama majeshi ya kukodi kwa ajili ya vurugu katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ofisi ya CCM Kata ya Nyakonga, wilayani Tarime, Mkoa wa Mara, Wasira amesema kuwa kila mara kunapokuwa na vurugu sehemu yoyote nchini, CHADEMA huwachukua vijana kutoka Tarime na kuwapeleka kufanya fujo katika maeneo mengine kama Mbeya.
Alienda mbali zaidi kwa kumtaja Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara, akidai kuwa kabla hajahamia CCM mwaka 2018, naye alikuwa sehemu ya mpango huo wa kuwasafirisha vijana kwa ajili ya vurugu.
“Kuna wakati kabla Waitara hajabatizwa, alipeleka vijana kufanya fujo, wakapata matatizo, na hata yeye mwenyewe akalazwa hospitalini. Baadaye akapona, akarudi, tukambatiza na kumpa kofia ya CCM,” amesema Wasira.
Ameongeza kuwa badala ya kujiingiza katika fujo zisizo na tija, vijana wa Tarime wanapaswa kutumia fursa zilizopo wilayani humo, ikiwemo sekta ya madini na kilimo, ili kujiletea maendeleo.
“Tarime tuna rasilimali nyingi; tuna madini, wachimbaji wadogo na ardhi yenye rutuba. Tuwasaidie vijana wetu kuzitumia fursa hizi badala ya kutumiwa na wanasiasa kwa maslahi yao,” amesisitiza.
Aidha, ameitaka CHADEMA kuacha mara moja kuchukua vijana wa Tarime kwa ajili ya vurugu, akisisitiza kuwa Tarime sio eneo la mapambano na vijana wake hawapaswi kukodishwa kwa ajili ya machafuko.