Rais wa Marekani Donald Trump amekataa kusema moja kwa moja kama uchumi wa nchi hiyo unakabiliwa na hali ya kuporomoka au kupanda kwa gharama za bidhaa, akieleza kuwa kuna “kipindi cha mabadiliko” kinachoendelea.
Akizungumza na waandishi wa habari, Trump ameulizwa iwapo anatarajia kushuka kwa uchumi mwaka huu, lakini alijibu kwa tahadhari, akieleza kuwa ni mchakato wa mabadiliko unaotokea katika sekta ya biashara na uwekezaji.
Hata hivyo, Waziri wa Biashara, Howard Lutnick, amekanusha uwezekano wa kuporomoka kwa uchumi wa Marekani, ingawa amekiri kuwa bei za baadhi ya bidhaa zinaweza kupanda kutokana na msukosuko wa sera za kibiashara.
Mjadala huu unajiri baada ya wiki yenye mabadiliko makubwa katika masoko ya fedha nchini Marekani, huku wawekezaji wakikumbwa na hali ya kutokuwa na uhakika kutokana na mabadiliko ya ghafla ya msimamo wa utawala wa Trump kuhusu ushuru kwa washirika wakubwa wa kibiashara wa Marekani.