Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza limewashtaki watu 47 kwa tuhuma za kukiuka sheria za zimamoto na uokoaji huku kesi tano zikiwa zimeshafikishwa mahakamani.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza, SSF. Elisa Mugisha amesema makosa yanayowakabili washitakiwa ni pamoja na kufanya biashara bila kuwa na cheti cha kuzuia majanga ya moto, kushindwa kutekeleza maagizo ya jeshi hilo na kujenga bila kupitisha ramani kwa idhini ya jeshi.
“Makosa yanayowapelekea kwenda mahakamani ningependa wananchi na umma wote wajue ni makosa ya kuvunja sheria za Zimamoto na Uokoaji kwahiyo mtu mmoja anaweza kuwa na tuhuma moja hadi tano na zilizonyingi ni kufanya biashara bila kuwa cheti cha majanga ya moto, pili kushindwa kutekeleza yale uliyoambiwa, lakini wengine ni wale ambao wanajenga bila kupitisha ramani au mali zao Jeshi la Zimamoto na Uokoaji,” amesema Mugisha
Hata hivyo Mugisha amesema miongoni mwa walioshtakiwa ni kampuni ya Imalaseko Investment, ambayo inamiliki sehemu ya mapumziko (resort), Mohamed Kumalija mmiliki wa Kumalija Lodge, Hamis Sudi na Robert Mageyane wote kesi zipo mahakamani.
“Miongoni mwa waliokamatwa ni kampuni ya Imalaseko Investment, ambayo inamiliki sehemu ya mapumziko (resort) na imekuwa ikisumbua jeshi hilo kwa miaka miwili. Kampuni hiyo ilishawahi kufikishwa mahakamani na jana ilihukumiwa tena kwa kukiuka sheria za zimamoto. Aidha, Mohamed Kumalija, mmiliki wa Kumalija Lodge, amefikishwa mahakamani kwa mara ya pili kwa kosa la kutosifu.
Mugisha amesema Jeshi hilo linawataka wananchi na wafanyabiashara kufuata sheria za zimamoto na uokoaji ili kuepuka hatua za kisheria.
“Tunawahimiza wote kushirikiana nasi kuhakikisha usalama wa maisha na mali zao,” amesema Mugisha