Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko anatarajia kuwa mgeni rasmi katika Jukwaa la Mwaka la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) ambapo zaidi ya washiriki elfu mbili kutoka nchi nzima watakutana kujadili namna ya kuboresha huduma zao kwa jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea jukwaa la mwaka la mashirika yasiyo ya kiserikali Jumatatu Septemba 2,2024 Jijini Dodoma Naibu waziri wa Maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi Maalum Mwanaidi Ali Khamis amesema kutakuwa na mafunzo kuhusu usimamizi wa miradi, uandishi wa maandiko dhana ya miradi, uandishi wa taarifa ya mfadhili na ufuatiliaji & tathmini.

“Lengo la majukwaa ya Mashirika yasiyo ya kiserikali katika ngazi za mkoa ni kubadilishana uzoefu fursa na changamoto katika utekelezaji wa shughuli za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, mafunzo ya kujengeana uwezo, utambuzi wa mashirika yaliyofanya vizuri na maazimio ya kushughulikia changamoto zilizoibuliwa”, ameeleza Mwanaidi.
Mwanaidi ameeleza kuwa Katika ngazi ya kitaifa siku ya kwanza yatafanyika mafunzo kwa Wasajili Wasaidizi na Wajumbe wa NaCoNGO wa Mikoa, Uzinduzi wa Madawati ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Sekta Binafsi na majadiliano ya pamoja na wadau wa Sekta Binafsi.
“Vilevile, kutakuwa na mafunzo kuhusu Usimamizi wa Miradi, Uandishi wa Maandiko Dhana ya Miradi, Uandishi wa Taarifa ya Mfadhili na Ufuatiliaji & Tathmini; Programu za Huduma za Kijamii kupitia Dhana ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) na Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC) katika eneo la Nkuhungu, Chamwino na Chang’ombe” amesema Mwanaidi.
Mbali na hayo Mwanaidi ametoa wito kwa wawakilishi wa wizara, idara na taasisi za kisekta, wajumbe wa bodi ya uratibu wa mashirika yasiyo ya kiserikali, wasajili wasaidizi wa mashirika yasiyo ya kiserikali, Wajumbe wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya kiserikali, wawakilishi wa sekta binafsi, washirika wa maendeleo, vyombo vya habari, mashirika yasiyo ya kiserikali, wanufaika wa miradi na afua zinazotekelezwa na mashirika yasiyo ya kiserikali, wananchi wa mkoa wa Dodoma na mikoa ya jirani, pamoja na jamii kwa ujumla, kushiriki katika jukwaa hilo kwa mustakabali wa sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali.
Naye Mchechemuzi kutoka shirika la World Vision Easter Mongi amesema kampeni hiyo kwa kushirikiana na maendeleo ya jamii inategemea kufanyika katika mikoa yote ya Tanzania ikianzia mikoa 16 ambako World Vision inapatikana.

“Tunashirikiana na Wizara 5 tukiamini kabisa wadau wote waliopo katika mikoa ambayo sisi hatupo wataenda kufanya ambacho sisi tunakifanya, lakini kampeni hii itadumu kwa miaka mitatu ilizinduliwa sasahivi hivyo ndani ya shirika tunategemea tuwe na bajeti isiyopungua dola milioni 3 katika kutekeleza kampeni hii,” amesema Mongi.
Mongi ameongeza kuwa, “Wadau tunaowategemea ni wote watakao kuwepo ukumbini na tuna amini wadau wa maendeleo, mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi binafsi watafanya kitu katika nyazifa zao ili kutokomeza utapiamlo Tanzania.”
Kauli mbiu katika jukwaa hilo ni “Mashirika yasiyo ya kiserikali ni wadau muhimu, washirikishwe kuimarisha utawala Bora”