Latest Posts

SERIKALI KUIMARISHA USHIRIKIANO NA ASASI ZA KIRAIA KATIKA MAENDELEO YA TAIFA

Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Asasi za Kiraia (AZAKI) nchini na haitakuwa kikwazo kwao katika shughuli zao za kuleta maendeleo.
 
Profesa Mkumbo alitoa kauli hiyo Septemba 9, 2024, wakati akifungua rasmi Wiki ya AZAKI jijini Arusha ambapo amesisitiza umuhimu wa AZAKI kushiriki katika kutoa mawazo yatakayosaidia kufungua fursa ndani na nje ya nchi.
 
Amesema ushirikiano kati ya AZAKI na serikali ni muhimu katika kushughulikia changamoto mbalimbali zinazoikumba jamii pamoja na kuzitumia fursa za masoko ya ndani na nje katika kukuza uchumi wa nchi.
 
Akizungumzia dira ya maendeleo ya taifa, Profesa Mkumbo alisema kuwa serikali inalenga kuhakikisha ustawi wa wananchi unafanikiwa ifikapo mwaka 2050.
 
Amesema ili kufikia malengo hayo, ni muhimu kujifunza kutoka kwa wananchi, kuwa wabunifu, na kushirikiana katika kuwekeza kwenye sekta muhimu kama elimu na miundombinu, hasa upatikanaji wa umeme wa uhakika kupitia mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere.
 
‘’AZAKI zihakikishe zinaisemea jamii  changamoto ambazo wanaziona na kutatuliwa ili kuisaidia serikali kuzishughulikia na si kuilalamikia kuwa haifanyi kazi ilihali hawajazibainisha ili zifanyiwe kazi na jamii iweze kupata mabadiliko’’, amesema Mkumbo.
 
Naye Rais wa Foundation For Civil Society (FCS), Dkt. Stigmata Tenga, amesisitiza umuhimu wa AZAKI katika kuleta mabadiliko ya kimaendeleo kwa wananchi, hasa katika sekta za afya, elimu, na miundombinu. Ameongeza kuwa rasilimali watu ni msingi wa maendeleo endelevu.
Mkurugenzi Mtendaji wa The Foundation for Civil Society (FCS) Justice Rutenge, akizungumza alipokuwa akitoa hotuba yake ya utangulizi wakati wa uzinduzi wa Wiki ya AZAKI, Jijini Arusha.
 
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa TradeMark Africa, Elibariki Shammy, amesema kuwa serikali ina mkakati wa kukuza biashara za kidijiti kwa kushirikisha vijana. Amebainisha kuwa vijana wanahitaji mazingira rafiki yatakayowawezesha kufikia mafanikio ya kiuchumi kupitia fursa zilizopo.
Mkurugenzi Mkazi wa Trademark Africa Elibariki Shammy, akizungumza katika mkutano huo.
Naibu Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU), Isabelle Mignucci, amesifu ushirikiano kati ya serikali ya Tanzania na mashirika mbalimbali akisema unaleta matokeo chanya katika maendeleo ya tekinolojia na ubunifu kwa vijana, hali ambayo inachangia katika ukuaji wa uchumi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!