Wazazi na walezi mkoani Mtwara wametakiwa kuacha kugharamia sherehe na badala yake wajikite zaidi kuwekeza katika elimu na kuwahamasisha vijana kupata elimu ili kukuza kizazi chenye maadili, maarifa na elimu kwa ujumla na kuepusha kuwa na kizazi kisicho na maadili mema.
Hayo yameelezwa na Mkoa wa Mtwara, Adam Khalfan kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Februari 21,2025 kwenye Masjid Salaam.
Ameongeza kuwa ili tuwapate viongozi katika jamii zetu lazima wazazi,walezi wagharamie na kuwekeza katika elimu kwakuwa ndio amri ya kwanza katika dini ya kiislamu ambayo unatakiwa kuitafuta kwa nguvu zote.

“Tumekuwa tukiwekeza kwenye sherehe za unyago na sherehe nyingine kwa gharama kubwa sana bila kuwekeza katika elimu,wenzetu wale wa Kanda ya Kaskazini wamefika pale walipofikia kwasababu wamewekeza katika elimu ukienda katika shule zetu utakuta wakuu wa shule si vijana wa Kusini,madaktari,kwenye benki na taasisi zingine hali ndio hiyo,hii ni kwasababu wazee wa Kaskazini waliwekeza katika elimu ili mwanadamu apate thamani ni lazima awe na Elimu.”Amesema Khalfani
Aidha kwa upande wake Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Jamaldin Salim amewataka waumini wa dini ya kiislamu kuhakikisha hawakubali kutenganishwa na vyama vya siasa au michezo na badala yake washikamane na kuwa kitu kimoja ili kufanya mambo ya kimaendeleo.
“Linapofika swala la Uislamu wote tuwe kitu kimoja,vyama vyetu visitutenganishe iwe vya siasa au vya mpira na hili ndio limenifanya kuzunguka kwenye misikiti ili kufikisha ujumbe huu na kukumbushana”Amesema Jamaldin
Pia amewataka waumini hao kuwaheshimu na kuwasikiliza viongozi wao hatakama kiongozi ana sifa duni na viongozi hao wahakikishe wanaishi kwenye njia za uadilifu, uaminifu na amewahimiza pia kutoa sadaka katika njia yenye kheri kwa ajili ya kuuinua uislamu.
Hata hivyo amewasihi watanzania kwa ujumla kuepuka kila aina ya jambo ambalo litapelekea kuvunja amani na utulivu katika kipindi cha uchaguzi.
“Tunaelekea kwenye kipindi cha uchaguzi mtu mwenye akili na busara anazingatia kwa jambo lilitokea kwa mwenzake hangojei limkute yeye,usingoje likupate ndio uanze kufikilia cha kufanya tunasikia baadhi ya nchi za wenzetu kupitia uchaguzi kuna tokea mambo mengi watu kupoteza mali,uhai na amani kupotea kwasababu ya uchaguzi.”Amesema Jamaldin