Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeeleza kuwa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Maporomoko ya Maji Duniani mwaka huu (International Waterfalls Day) kitafanyika tarehe 16 Juni 2025 katika Hifadhi ya Mpanga Kipengere, iliyopo mikoa ya Njombe na Mbeya.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano cha TAWA, maadhimisho ya mwaka huu yamepewa hadhi ya “Maporomoko ya Maji ya Dhahabu – Msimu wa Tatu (Golden Waterfalls Season 3)”, kutokana na hifadhi hiyo kubainisha zaidi ya maporomoko ya maji 50 – idadi ambayo ni kubwa kuliko hifadhi yoyote barani Afrika.

“Ni Maporomoko ya Dhahabu kwa sababu ya kuthamini juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza utalii, ambapo serikali yake imefanya maboresho makubwa ya miundombinu ya utalii katika hifadhi hii ndani ya miaka minne iliyopita,” imeeleza taarifa hiyo.
Katika kilele hicho, TAWA imepanga kuzindua rasmi utalii wa “Bustani ya Dunia”, eneo lenye mandhari ya kipekee likiwa na visiwa vya msitu, zulia la maua mwitu zaidi ya aina 400, utalii wa baridi, utalii wa mbio za milimani pamoja na huduma za natural therapy tourism.

Watalii watapata fursa ya kushuhudia Maporomoko ya TAWA, Glory na Minde, pamoja na kutembelea bustani yenye kiyoyozi asilia. Pia watapata ladha ya kipekee kutokana na mchanganyiko wa kanda tatu za ikolojia zenye hali ya joto, wastani na baridi – hali inayovutia shughuli za kuogelea na matembezi ya kitalii.
“Ni kwa mara ya tatu sasa maadhimisho haya yanafanyika Hifadhi ya Mpanga Kipengere tangu mwaka 2023, ikiwa ni sehemu ya kukuza utalii wa ndani na kimataifa kupitia vivutio vya asili,” imeongeza taarifa hiyo.
