Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kushughulikia upatikanaji wa huduma za kijamii katika sekta ya afya, maji, na umeme kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na sera zinazomlenga mwananchi.
Akizungumza wakati akiwasilisha hotuba ya Tanzania katika Kikao cha 61 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika Geneva, Uswizi, Waziri Homera alisema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaweka mkazo katika kuboresha huduma za jamii, utawala bora na maendeleo jumuishi ili kulinda utu na ustawi wa wananchi.
Alieleza kuwa hatua hizo zinajumuisha uzinduzi wa Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050, utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Bima ya Afya kwa Wote, pamoja na kuimarishwa kwa miundombinu ya afya, maji na umeme ili kupunguza umaskini na kuongeza fursa za kiuchumi.
Katika kukuza usawa wakijamii Waziri Homera ameweka bayana kuwa Serikali inatekeleza miradi ya kimkakati ikiwemo Mradi wa Umeme wa Maji wa Mwalimu Julius Nyerere, pamoja na sera ya elimu bila malipo na ongezeko la wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu.
Aidha katika kujenga Taifa lenye umoja na ushirikiano Serikali imeanzisha Wizara ya Maendeleo ya Vijana ili kuimarisha ushiriki wa vijana katika maendeleo, huku ikijidhatiti kutekeleza programu za kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto na kuboresha upatikanaji wa haki kupitia akampeni ya Msaada wa Kisheria na matumizi ya mifumo ya kidijitali katika sekta ya haki.
Waziri Homera alisisitiza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na jumuiya ya kimataifa katika kukuza na kulinda haki za binadamu kupitia mazungumzo, ushirikiano na kuheshimu misingi ya Haki za Binadamu.